Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
WASANII mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya, wakiongozwa na Maua Sama pamoja na Chege chigunda wamekonga nyoyo za wanamichezo wa UMISSETA na kuleta hamasa kubwa kwa wadau michezo mkoa wa Mtwara walipotumbuiza jukwaani leo kwenye ufunguzi wa Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA).
Mashindano hayo yaliyofunguliwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Caroline Nombo kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Katika ufunguzi huo vikundi mbalimbali vya kwaya na ngoma vimetumbuiza na kuufanya umati wa watazamaji kupanda jukwaani na kuimba pamoja na wasanii mbalimbali waliokuwa wakitumbuiza.
Akisoma hotuba ya ufunguzi wa mashindano hayo Profesa Nombo amepongeza ubunifu wa waandaji wa mashindano ya mwaka huu kwa kuwashirikisha wasanii ili kuja kutoa burudani na kuonesha vipaji na vipawa walivyopewa na Mwenyezi Mungu.
“Ninawashukuru na kuwapongeza wasanii mbalimbali wanaoendelea kusherehesha wakiwemo Maua Sama na Chege. Wanahabari na wasanii hawa wanasaidia kuitangaza michezo hii na wameongeza hamasa kwa jamii kuifuatilia nchi nzima wakiwemo wazazi, walezi wa wanafunzi pamoja na Viongozi wa Vyama vya Siasa na viongozi wa Serikali popote walipo,” amesema Profesa Nombo.
Profesa Nomba alitumia ufunguzi wa mashindano haya kuwaagiza wadhibiti ubora wa Shule kote nchini kuanzia ngazi ya wilaya, kanda na Makao makuu ya Wizara kufanya tathmini na kutoa ushauri wa kuimarisha ufundishaji wa michezo, elimu kwa michezo na sanaa katika taasisi zote hapa nchini
Amesema michezo ya UMISSETA na ile ya vyuo vya ualimu (UMISAVUTA) imekuwa ikiibua vipaji vya wanamichezo wengi ambao miongoni mwao wamefanikiwa kung’ara kitaifa na kimataifa, kutokana na hilo Serikali imeamua kurejesha mashindano yaVyuo vya Ualimu pia kwa kuzingatia agizio la Mkuu alilolitoa mwaka 2019 wakati wa kufungua mashindanio ya UMISSETA na UMITASHUMTA la kutaka mashindano hayo yarejeshwe.
Mashindano yameandaliwa na Wizara tatu zinazohusika na Elimu, Michezo na TAMISEMI chini ya Kamati ya Uratibu ya Kitaifa ya Makatibu Wakuu wa Wizara hizo.
Mbali na hivyo, Mashindano hayo yalitanguliwa na Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) yaliyofunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa Juni 8, mwaka huu mjini Mtwara na kufungwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul Juni 18.Mashindano ya UMISSETA yanatarajiwa kufungwa rasmi Julai 3, mwaka huu.
%%%%%%%%%%%%%
More Stories
GETHSEMANE GROUP KINONDONI yaja na wimbo wa siku yetu kwaajili ya harusi
Startimes yazindua makala ya China, Africa
Mwanasheria wa Katavi aliyetimkia kwenye muziki achaguliwa tuzo za MIEMMA