November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Matumaini ya vijiji 16 kupata maji ya bomba Chunya yarejea

Na Esther Macha,Timesmajira,Online,Chunya

MATUMAINI ya wananchi wa vijiji 16 wilayani Chunya kupata maji ya bomba yamefufuka baada ya Serikali kutoa zaidi ya sh.bilioni 2.6 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa mradi wa bwawa la matwiga ambao ulikwama kukamilika kwa zaidi ya miaka 16.

Mradi wa Bwawa la Matwiga ambao ulianza kujengwa miaka 16 iliyopita kwa lengo la kuhudumia wananchi wa vijiji 16 wapate maji safi na salama, ulikwama kukamilika kutokana matumizi mabaya ya fedha.

Hali ambayo ilipoteza matumaini ya wananchi hao, lakini sasa Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kuufufua kwa kutoa sh. bilioni 2.6 .

Akizungumza wakati wa kukagua mradi huo Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprsca Mahundi, amesema wananchi wahakikishe wanatunza mradi huo vizuri ili uweza kusaidia upatikanaji wa maji .

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprsca Mahundi (aliyeshika chepe) akichanganya zenge alipokagua ujenzi wa mradi huo.

Meneja wa Wakala wa Usamabazaji wa Maji Vijijini, (RUWASA) wilaya ya Chunya Mhandisi Nassoro Ismail, amesema mradi huo umeanza kutekelezwa Septemba 30, mwaka huu na kwamba unategemewa kukamilika Machi 30, mwakani na kuwa hadi sasa mradi umetekelezwa kwa asilimia 20.

Amesema mradi huo ukikamilika utaweza kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa asilimia 8 na kwamba awamu kwanza itahudumia vijiji viwili vya Matwiga na Isangawana vyenye idadi ya wakazi wapatao 13,000 pia awamu ya pili itakuwa kwa vijiji vya Mazimboe na Mtanila.

Mmoja wa wanachi wa Kata ya Matwiga, Haruna Ngogo amesema walikuwa wanasubiri mradi huo kwa nguvu zote kwani wana kiu na kushukuru Serikali kwa kufufua upya matumaini ya wao kupata maji safi na salama.

Tanki la kuhifadhi maji likiwa hatua za mwisho za ujenzi. Picha zote na Esther Macha.

Naye Mbunge wa Lupa, Masache Kasaka mbali ya kuipongeza serikali amesema wananchi waulinde mradi huo.

Aidha Mkurugenzi wa Wakala wa Maji nchini Clement Kivegalo amesema mabomba yote yametengenezwa nchini na yamefika eneo la mradi.