Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
JUMLA ya matukio 16,455 ya vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto yameripotiwa katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya Mkoani Tabora katika kipindi cha mwezi Januari hadi Disemba 2022.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian alipokuwa akihitimisha sherehe za kilele cha siku ya wanawake duniani zilizofanyika juzi Kimkoa wilayani Urambo.
Alisema vitendo hivyo vinajumuisha matukio 3,646 ya ukatili wa kimwili, 2,549 wa kingono na 10,260 wa kisaikolojia na kubainisha kuwa matukio hayo hayakubaliki hata kidogo na hayana afya kwa jamii.
Alisisitiza kuwa serikali ya awamu ya 6 imejidhatiti kikamilifu kudhibiti ukatili wa aina yoyote ile kimwili, kisaikolojia, kingono na kiuchumi hivyo akatoa wito kwa jamii kushirikiana na serikali kwa kufichua wale wote wanaofanya vitendo hivyo.
Balozi Batilda alifafanua kuwa katika kukabiliana na vitendo hivyo serikali imetunga sera, sheria na miongozo kama vile Mpango Kazi wa kutokomeza vitendo vya ukatili (MTAKUWWA) na uwepo wa madawati ya jinsia na watoto katika vituo vyote vya polisi.
Alitaja mkakati mwingine kuwa ni kuanzishwa kwa sheria ya msaada wa kisheria pamoja na kampeni mbalimbali za utoaji elimu kwa umma juu ya kuzuia na kufichua vitendo vya ukatii katika jamii
Alionya watu au kikundi cha watu kitakachobainika kueneza mambo yasiyofaa na yaliyo kinyume na maadili au utamaduni wa nchi na yaliyo kinyume na maandiko matakatifu, huku akipongeza viongozi wa dini kwa kuendelea kukemea kwa nguvu vitendo vya ushoga ambavyo vinaonekana kushamiri katika nchi mbalimbali.
‘Ndugu zangu serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni sikivu na inaheshimu na kusimamia maadili ya Kitanzania, ipo macho na haitaruhusu hata kidogo mambo yaliyo kinyume na maadili kuharibu maisha ya vijana wetu’, alisema.
Batilda alipongeza hamashauri za Mkoa huo kwa kuendelea kutekeleza maelekezo ya serikali ya kuwezesha wanawake kiuchumi, ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 jumla ya vikundi 1,968 vilisajiliwa katika mfumo na vikundi 229 (wanawake 112, vijana 75 na walemavu 34) kukopeshwa kiasi cha sh bi 2.02.
Aidha alizitaka kuanzisha na kusimamia uendeshaji wa majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi kwa kutenga bajeti ili yaweze kutimiza majukumu yao ikiwemo kuanzishwa Vituo vya Mkono kwa Mkono (One-Stop Centre) ili kurahisisha utoaji huduma kwa waathirika wa ukatili.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu