Na Joyce Kasiki,Timesmajira Online, Dodoma
TUME ya Taifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (COSTECH), imeandaa semina kwa watafiti kutoka sekta ya afya, mifugo, kilimo na maliasili kwa lengo la kuwaleta pamoja na kutoa matokeo ya utafiti, walioufanya katika maeneo mbalimbali ili waweze kuishauri serikali .
COSTECH imeanza semina hiyo kwa kuwakutanisha pamoja watunga sera, watafiti, watu wa mipango na watoa maamuzi kutoka katika sekta ya afya.
Akifungua semina hiyo iliyofanyika jijini hapa Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Zabron Katale amesema jukumu la Tume hiyo ni kuhakikisha matokeo ya tafiti mbalimbali zinazofanywa nchini, yanatumika katika kutunga sera na katika mipango mbalimbali ya maendeleo ya nchi badala ya kuwekwa kwenye makabati.
Hata hivyo, Dkt. Katale ambaye ni Mkurugenzi wa Uratibu na Uendelezaji wa Tafiti wa COSTECH, amesema kuna changamoto ya tafiti nyingi kuwekwa kwenye makabati badala ya kutumika katika kutung sera na kwenye mendeleo kwa ujumla.
Akitoa mada kuhusu matokeo ya tafiti na mchango wake kwenye maendeleo ya nchi Kaimu Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maarifa wa COSTECH, Dkt. Philbert Luhunga amesema kazi ya matokeo ya utafiti ni kuwezedha nchi kufikia malengo 17 ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030.
“Ili tufanikiwe, lazima tutumie matokeo ya utafiti katika kutunga sera ndiyo maana tunahimiza matokeo ya utafiti yatumike kwenye kutunga sera, mipango ya maendeleo katika sheria, taratibu na muongozo,” amesema.
Amesema serikali inataka matokeo ya utafiti, yatumike ili kubadilisha jamii huku akisema changamoto ipo kwa watafiti wenyewe katika utekelezaji wa tafiti wanazozifanya.
“Kwa mfano, yapo mambo mengi ambayo Wabunge wamekuwa wakizungumza wawapo bungeni, watafiti wanapaswa wayafanyie utafiti masuala muhimu na kuyatolea matokeo kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla,” amesema na kuongeza;
“Na hii ndiyo kazi ya COSTECH, inawaleta pamoja watafiti na kuwaunganisha na watunga sera ili kuwe na muunganiko na kuwezesha matokeo ya watafiti kuwafikia watunga sera”.
Naye Ofisa Mtafiti Kiongozi wa COSTECH upande wa Afya, Dkt. Khadija Malima amesema katika kufanya utafiti lazima kuwe na ushahidi wa kisayansi unaozingatia weledi, ili uweze kutoa matokeo yaliyokusudiwa.
Amesema nchi inataka matokeo ya uhakika kwa ajili ya kupangia mipango ya maendeleo ya nchi na kufikia malengo ya dira ya mendeleo ya taifa na si tafiti za kukaa vitabuni.
“Wabunge ndiyo watunga Sera, kwa hiyo watafiti ndiyo wanaoweza kulisaidia Bunge ili liwe na taarifa za uhakika za kuwasaidia Wabunge kutunga sera, lazima watafiti mtumie nafasi yenu bila hivyo mambo hayataenda,” amesema.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi