November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Matokeo Uchunguzi wa sampuli kulinda afya za wananchi

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

KATIKA kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024 Mamlaka ya Mkemia Mkuu ilikuwa imefanyia uchunguzi sampuli 141,683 kati ya sampuli 145,273 zilizopokelewa katika kipindi hicho.

Akizungimza bungeni jijini Dodoma leo Mei 13,2024 wakati akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ,Waziri wa wizara hiyo Ummy Mwalimu amesema sampuli zilizofanyiwa uchinguzi ni sawa na asilimia 97.6 kwa sampuli zilizopokelewa.

Aidha amesema sampuli zilizofanyiwa uchunguzi ni sawa na ongezeko la asilimia 43 ikilinganishwa na sampuli 99,159zilizochunguzwa kwa kipindi kama hicho cha Mwaka wa Fedha 2022/23.

” Matokeo ya uchunguzi huo yalisaidia Serikali na Mamlaka nyingine za usimamizi
na udhibiti kufanya maamuzi stahiki katika kulinda afya za wananchi na mazingira pamoja na utoaji wa haki katika vyombo vya maamuzi. ” amesema Waziri Ummy

Vile vile amesema katika kuhakikisha ubora wa matokeo ya uchunguzi yanayokubalika kitaifa na kimataifa, Mamlaka imepata Ithibati ya Mifumo ya Ubora ya Maabara (ISO17025:2017) katika Maabara ya Sayansi Jinai Toksikolojia.

Wakati huo huo amesema,katika kuchangia utoaji wa haki katika vyombo vya maamuzi kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, Mamlaka ilitoa ushahidi
wa kitaalam mahakamani kwa mashauri 882 sawa na asilimia 71.4 ya lengo la kutoa ushahidi wa mashauri 1,236.

“Aidha, kulikuwa na ongezeko la asilimia 117 ikilinganishwa na mashauri 407 yaliyotolewa ushahidi mahakamani kwa kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2022/23.”amesema

Kwa mujibu wa Ummy ,mafanikio haya yamechangiwa na Mfumo wa Kielekitroniki wa Kuratibu Taarifa za Wataalam Watoa ushahidi Mahakamani .

Vile vile amesema Mamlaka ilisajili wadau 974 wanaojishughulisha na biashara ya kemikali sawa na asilimia 82.8 ya lengo la kusajili wadau 1176. Wadau waliosajiliwa waliongezeka kwa asilimia 33.2 ikilinganishwa na Wadau 731 waliosajiliwa kwa kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha 2022/23.

Ummy amesema ,lengo la kusajili wadau hawa ni kuendelea na juhudii za kulinda afya, mazingira na usalama wa nchi dhidi ya kemikali hatarishi na bashirifu zinazotumika
kutengeneza dawa za kulevya au silaha za kemikali.

Mbali na hayo Umny amesema Mamlaka pia ilitoa mafunzo kwa jumla ya madereva 2,961 juu ya usafirishaji salama wa Kemikali nchini ambayo yamesaidia kuwapa uelewa wa namna bora ya kujilinda, kulinda watu wengine pamoja na kulinda mazingira wakati wa usafirishaji wa kemikali hizo.

Amebainisha kuwa,katika kuhakikisha kuwa Mamlaka inakuwa na Vifaa vya kutosha kulingana na mahitaji na vyenye teknolojia ya kisasa, Serikali imeiwezesha Mamlaka kununua mitambo mikubwa mitatu (3) aina ya Gas Chromatography Mass
Spectrometer (GC-MS/MS), MinLab 153 (OSA4) na Gas Chromatography (GC) pamoja na vifaa vingine vya maabara vyenye thamani ya Shilingi Bilioni 4.57.

Amesema uwekezaji huo umeiwezesha Mamlaka kuwa na ufanisi na kuendelea kusogeza huduma karibu zaidi kwa wananchi.