Na Jackline Martin, TimesMajira Online
Idadi ya watalii walioingia nchini waliotembelea vivutio mbalimbali vya Utalii katika kipindi cha Januari hadi Mei 2022 wameendelea kuongezeka hadi 458,048 ikilinganishwa na watalii 317, 270 walioingia nchini mwaka 2021 ikiwa ni sawa na asilimia 44.4
Akizungumza na waandishi wa habari jana (Julai 14, 2022), Kaimu Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi, Daniel Masolwa alisema idadi kubwa ya watalii wanaoingia nchini ni matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na Rais Samia Suluhu na kupitia Filamu ya Tanzania the Royal Tour iliyozinduliwa nchini kwa mara ya kwanza jijini Arusha Aprili 25, 2022
“Filamu ya The Royal Tour imeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya Utalii ambapo kwa sasa Tanzania inashuhudia ongezeko kubwa la watalii, kati ya watalii 458,048 walioingia nchini, Watalii 137,758 waliingia nchini kupitia Zanzibar ambao ni sawa na asilimia 30.1 ya watalii wote.”
Aidha Masolwa alisema Ufaransa iliongoza kwa idadi kubwa ya watalii walioingia nchini Januari hadi Mei 2022 kwa mchanganuo wa Utaifa;
“Idadi ya watalii walioingia nchini kutoka nchi zilizo nje ya Bara la Afrika kwa mchanganuo wa Utaifa katika kipindi cha Januari hadi Mei 2022 unaonesha kuwa Ufaransa iliongoza kwa idadi kubwa zaidi ya watalii 28,115 ikifuatiwa na Poland ikiwa na watalii 22,651 ambapo nchi nyingine ni Marekani (21,661), Ujerumani (16,527), Uingereza (14,136) na India (13,641)”
Masolwa alisema Idadi kubwa ya watalii walioingia nchini kutoka nje ya Bara la Afrika kwa Mwezi Mei 2022 peke, waliotoka Marekani (5,606), Ufaransa (4,456), India (4,211), Uingereza (3,294) na Ujerumani (3,160)
Pia Masolwa alizungumzia hali ya upatikanaji huduma pale watalii wanapofika nchini ambapo amezitaka sekta binasfi wajipange kukabiliana na idadi ya watalii wanaoingia ili kuwapa huduma wanazozitaka lakini pia watalii wazidi kuendelea kuja nchini kufanya utalii
Mbali na hayo Masolwa alisema kwa mujibu wa sera ya Mapitio ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu, takwimu za Idadi ya watalii wanaoingia nchini zinaweza kufanyiwa mapitio endapo takwimu mpya na zilizohusishwa kutoka kwenye chanzo zitapatikana.
Kupitia fursa hiyo Masolwa amewaomba watanzania kushiriki kikamilifu katika Sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 23, 2022;
“Taarifa zitakazokusanywa katika sensa zitahusu idadi ya watu na miongoni mwa taarifa hizi pia tutapata watalii vilevile kujua idadi ya nguvu kazi, ukubwa wa soko kutokana na idadi ya watu hivyo tushiriki kwa kutoa taarifa sahihi ili nchi iwe katika nafasi nzuri ya kupanga vizuri mipango mbalimbali ya maendeleo”
More Stories
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili