NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, KISARAWE
BODI
ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (Gaming Board of Tanzania-GBT) imeteketeza
mashine haramu za kuendeshea michezo ya kubahatisha (Slot Machines) zipatazo
300.
Sambamba
na hilo watu Wanane (8) wako mikononi mwa vyombo vya kisheria wakihusishwa na
mashine hizo.
Zoezi
hilo lililoongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa GBT Bw. James Mbalwe limefanyika
Oktoba 28, 2022 kwenye eneo la kuteketeza vifaa vya kielektroniki lililoko Wilayani
Kisarawe Mkoani Pwani.
“Katika
jitihada za kudhibiti waendeshaji haramu wa michezo ya kubahatisha GBT
iliendesha operesheni maalum kwenye mikoa ya Pwani, Lindi, Kilimanjaro, Dar es
Salaam, Morogoro, Manyara na Songwe na kufanikiwa kukamata mashine hizo zenye
thamani ya shilingi Milioni 300.” Alifafanua Bw. Mbalwe.
Alisema
mashine hizo zilikamatwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kufanya biashara
bila ya Leseni ya GBT, mashine kuingizwa nchini bila ya kufuata taratibu za
kisheria, kufanya biashara kwenye maeneo ambayo hayaruhusiwi au hayajakaguliwa
na kuthibitishwa na Bodi (GBT) pamoja na
kukwepa kulipa kodi na tozo mbalimbali.
“Mashine
hizi pekee zimepelekea serikali kukosa mapato yake kiasi cha shilingi Milioni
33 kwa mwezi sawa na shilingi Milioni 400 kwa mwaka, jambo hili halikubaliki.”
Alisisitiza.
Pia
Bw. Mbalwe alisema waendeshaji hao haramu ndio ambao wamekuwa wakiruhusu watu
wenye umri usioruhusiwa kucheza michezo hiyo,
“Operesheni
hii ni endelevu na itakuwa ikifanyika mara kwa mara ili kudhibiti vitendo hivyo
na kuhakikisha michezo ya kubahatisha inaendeshwa kwa kuzingatia misingi ya
kisheria na kuleta tija katika maendeleo ya Taifa letu bila ya kusababisha
athari hasi au madhara yoyote kwa jamii yetu.” Alisisitiza.
Aidha
Mkurugenzi Mkuu huyo aligusia pia hatua ya hivi karibuni ya Mkuu wa Wilaya ya
Shinyanga Mhe. Yasinta Mboneko ya kuzuia biashara ya michezo ya kubahatisha
katika wilaya yake baada ya kubaini kwamba kulikuwa na uvunjfu wa sheria ambapo
alielekeza jeshi la jadi Sungusungu kusimamia agizo hilo.
“Sisi kama chombo cha serikali chenye dhamana ya kusimamia michezo ya kubahatisha, tunaona hatua aliyochukua ni nzuri na itasaidia katika kuimarisha utekelezaji wa sheria, lakini nashauri wakati mwingine ili zoezi hilo lifanyike vizuri ni vema viongozi na mamlaka nyingine wakashirikisha GBT ambayo ina watu wenye weledi katika eneo hilo na kwahakika itarahisisha utekelezaji wake bila ya kuleta taharuki.” Alisema.
Alisema “GBT tumeamua kupambana na uhalifu wa mashine za michezo ya kubahatisha zilizozagaa
kwenye maeneo yasiyoruhusiwa na kutozingatia sheria, hata kama watakuwa ni
waendeshaji tuliowapa leseni tutachukua hatua kali pindi tutakapobaini
wamevunja sheria.” Alionya Bw. Mbalwe.
Pia
alisema GBT inaendelea na msako wa kuwabaini wale wote wanaoingiza mashine hizo
nchini kinyume cha sheria.
Nae
Mkurugenzi Msaidizi wa Kampuni ya Chilambo ambayo ndiyo inahusika na kuharibu
“taka hatarishi” hususan za umeme, Bi. Venither Gideon alisema mashine hizo
zitavunjwa vunjwa na kisha kuzitenga kwenye makundi kulingana na asili yake.
“Jukumu letu ni kuhakikisha tunaziharibu mashine hizi katika njia ambayo ni salama kwa uhifadhi wa mazingira.” Alisema.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam