November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mashindano ya Wavu Kanda ya Tano sasa ni Machi, 2021

Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online

MICHUANO ya Kanda ya Tano ya Afrika ya Wavu Ukukweni hatua ya pili ya kutafuta nafasi za kufuzu kushiriki mashindano ya Olimpiki ‘Africa sub Zonal V Olympic qualifiers’ sasa ni rasmi yatafanyika mwishoni mwa mwezi Machi 2021.

Awali michuano hiyo ilipangwa kufanyika Machi 26 hadi 30 mwaka huu katika fukwe za Coco lakini yaliahirishwa kutokana na mlipuko wa Covid-19.

Kabla ya kuahirishwa kwa mashindano hayo, Shirikisho la Mpira wa Wavu Barani Afrika (CAVB) liliiteua Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo ambapo ilipangwa kundi B pamoja na timu za Taifa za Ghana, Afrika Kusini, Sudan na Niger.

Uwenyeji huo uliifanya Tanzania kuungana na mataifa mengine manne yaliyopewa uwenyeji wa kuandaa mashindano hayo lakini pia ikiwa ni mara ya pili ndani ya mwaka huu kupewa uwenyji wa michuano mikubwa baada ya Januari mwaka huu kuandaa michuano ya Kanda ya Tano ya Afrika kwa upande wa wanawake yaliyofanyika Januari 9 hadi 13 katika fukwe za Mbalamwezi jijini Dar es Salaam.

Ikumbukwe kuwa, kikosi cha Tanzania kilichokuwa kinaundwa na Ford Edward na David Neek huku kile cha pili kikiundwa na Shukuru Ally na Said Alhaj kilifanikiwa kufuzu hatua hiyo ya pili baada ya kufanikiwa kufanya vizuri katika mashindano ya awali yaliyofanyika katika fukwe za Lido zilizopo Entebbe, Uganda kuanzia Desemba 18 hadi 22, 2019.

Ushindi walioupata Tanzania dhidi ya Uganda, Kenya na Sudan kuliwafanya kukaa juu ya msimamo wa kundi lao wakifuatiwa na Kenya ambao nao walifuzu kutinga hatua ya pili huku Sudan wakishika nafasi ya tatu na Uganda wakikaa nafasi ya mwisho.

Akizungumzia mashindano hayo katika ufunguzi wa mafunzo ya ndani ya kitaifa ya waamuzi wa mpira wa wavu ( National and Candidate Referee course), Katibu mkuu wa Chama Cha Mpira wa wavu Tanzania (TAVA) ambaye pia ni mkufunzi wa kwanza wa makocha wa mpira wa Wavu na Wavu Ufukweni kutoka Tanzania na Afrika kwa ujumla Alfred Selengia ameuambia Mtandao huu kuwa, baada ya kuahirishwa kwa michuano hiyo walikuwa wakisubiri kwa hamu tarehe nyingine ya mashindano hayo.

Amesema, kutangazwa kwa tarehe hiyo pia kunawapa nafasi ya kuanza mapema mipango ya kuangalia ni namna gani wataweza kufanya vizuri ili kuiwakilisha nchi katika mashindano ya olimpiki.

“Tayari tarehe zimepangwa upya na michuano itafanyika mwezi Machi, 2021 hivyo moja ya mpango ambao tunao ni kikosi chetu cha timu ya Taifa kuingia kambini mwishoni mwa mwezi Januari,” amesema Selengia.

Pia kutokana na wachezaji kutokuwa sawa kisaikolojia baada ya kuahirishwa kwa michuano hiyo, watahakikisha wanakaa mapema kuwaweka sawa kwani baadhi yao wameshaanza mazoezi ya mmoja mmoja na wapo tayari kuhakikisha wanabakiza kombe nyumbani.

Hata hivyo, Selengia amewaomba wadhamini kujitokeza kudhamini michuano hiyo na kuacha kutupia macho mchezo wa mpira wa miguu pekee kwani kuna fursa nyingi zinazopatikana katika michezo mingine.

Kwa upande wake Rehema Juma ambaye ni Mkufunzi wa mchezo wa wavu amesema, mafunzo ya mwaka huu yameandaliwa vizuri na yatakuwa na tija kubwa kwenye sekta ya uamuzi wa mchezo wa wavu nchini Tanzania.

Pia amewataka Wanawake kujitokeza kwa wingi kushiriki mafunzo hayo kwani kumekuwa na muitikio mdogo wa wanawake kwenye masuala ya michezo na kuachana na dhana michezo ni kwa wanaume pekee.