December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mashindano ya umitashumta taifa kuanza kutimua vumbi Juni,3,2023

Na Allan Vicent, Timesmajira online,Tabora

MASHINDANO ya Taifa kwa wanafunzi wa shule za msingi nchini (UMITASHUMTA) yanatarajia kuanza kutimua vumbi Juni 3,mwaka huu katika viwanja vya shule ya sekondari ya wavulana na ya wasichana Tabora.

Akizungumza na vyombo vya habari Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt.Batilda Burian amesema maandalizi ya michuano hiyo yamekamilika kwa asilimia 100 na timu za mikoa yote 31 kutoka Tanzania Bara na Visiwani tayari zimewasili.

Amebainisha kuwa jumla ya wanamichezo 10,000 wakiwemo walimu, madaktari, viongozi na wanafunzi wanatarajiwa kushiriki mashindano hayo ambayo yamepata hamasa kubwa kutoka kwa wapenzi wa michezo mkoani hapa.

Batilda ameongeza kuwa mashindano hayo ambayo yanafanyika kwa mwaka wa pili mfululizo mkoani hapa ni fursa muhimu sana ya kiuchumi kwa wananchi wake hivyo akawataka kupokea na kuhudumia vizuri wageni wote katika maeneo yao.

Ametaja baadhi ya michezo itakayoshindaniwa kuwa ni pamoja na mpira wa miguu kwa wanawake na wanaume, mpira wa mikono, pete (netball), kikapu, wavu (volleyball), riadha, soka maalumu ya walemavu na sanaa za ndani.

Amebainisha kuwa mashindano hayo ambayo yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi Juni 6 mwaka huu na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Isdori Mpango na kufikia tamati Juni 13.

Ameongeza kuwa mashindano hayo yatafuatiwa na yale ya shule za sekondari (UMISSETA) ambayo yatafanyika katika viwanja hivyo hivyo na uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ambao utatumika kwa uzinduzi na ufungaji mashindano hayo.

Aidha ameeleza kuwa takribani wanamichezo 7,600 wanatarajiwa kushiriki katika mashindano ya UMITASHUMTA na idadi kama hiyo kwenye mashindano ya UMISSETA ambayo yanatarajiwa kuanza Juni 15 na kuhitimishwa Juni 25.

‘Tunamshukuru sana mama yetu Rasi Samia kwa kutenga zaidi ya milioni 800 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya viwanja vya michezo katika shule mbalimbali ikiwemo shule 2 za Mkoa wa Tabora ya wavulana na wasichana,”amesema.

Balozi Batilda amebainisha kuwa baada ya kumalizika mashindano hayo baadhi ya wachezaji watateuliwa ili kuunda kikosi kitakachowakilisha nchi katika mashindano ya shule za msingi na sekondari kwa nchi za Afrika Mashariki (FEASSSA).