Na Rose Itono, TimesMajira Online
KAMPUNI ya The Look inayoandaa mashindano ya kumsaka mrembo, imezindua rasmi mashindano ya kumtafuta miss Tanzania 2021, huku ikiitaka jamii kumpata mrembo atakayeishi bila kuwa na skendo mbaya, badala yake kuwa kiongozi bora wa baadaye katika taifa hili.
Mbali na hivyo, pia imewapa semina mawakala wa mashindano hayo kutoka mikoa mbalimbali ili kuwawezesha kushiriki vyema kwenye kinyang’anyiro cha kumpata mrembo huyo, atakayeliwakilisha Tanzania kwenye kinyang’anyoro cha kumsaka mrembo wa dunia.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo leo, Mkurugenzi wa The Look Basila Mwanukuzi amesema, tangu kampuni hiyo ianze kuandaa mashindano hayo mwaka 2018 hakuna mrembo yeyote aliyeshinda nafasi hiyo na kupata skendo mbaya.
“Tangu kampuni yangu ianze rasmi kuandaa mashindano ya Miss Tanzania mwaka 2018, hakuna mshindi yeyote aliyewahi kuwa na skendo tofauti na awali ambapo kuna baadhi ya washindi waliitumia nafasi yao vibaya kwa kushindwa kuwa mabalozi wazuri hapa nchini, kutangaza urembo na utalii,” amesema Mwanukuzi.
Mwanukuzi aliyataja malengo makubwa ya kuandaa mashindano hayo kuwa, ni pamoja na kuhakikisha mshindi anautangaza utalii wa ndani, kukuza sanaa ya urembo nchini na kuinua vipaji vyao, pia wamelenga kuwajenga wasichana waweze kujiamini na kila mrembo aweze kufanya kazi za kijamii kwa kuwa na programu au miradi itakayowezesha kusaidia Jamii.
Hata hivyo, amempongeza rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kushika wadhifa wa juu na kumuahidi kuendeleza kuutangaza utalii wa ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake mshindi wa Miss Tanzania 2020 Slivia Sebastian amesema, kikubwa kinachotakiwa katika kufanikisha mashindano hayo ni ushirikiano ili wasichana waweze kutimiza ndoto zao.
Jumla ya mawakaka kadhaa kutoka mikoa mbalimbali walishiriki semina hiyo huku wakiahidi kutoa ushirikino ili kumpata mrembo atakayewakilisha Tanzania kwenye mashindano ya dunia(miss world).
%%%%%%%%%%%%%
More Stories
GETHSEMANE GROUP KINONDONI yaja na wimbo wa siku yetu kwaajili ya harusi
Startimes yazindua makala ya China, Africa
Mwanasheria wa Katavi aliyetimkia kwenye muziki achaguliwa tuzo za MIEMMA