Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
MASHINDANO ya mchezo wa Kabaddi Afrika yaliyopangwa kuanza kutimua vumbi Desemba 11 hadi 15 mwaka huu hapa nchini, sasa yamesongezwa mbele hadi Februari, 2021.
Katika mashindano hayo ya Afrika mwenyeji Tanzania atawakilishwa na timu ya wanaume na wanawake ambazo zitachuana na timu kutoka nchini Kenya, Cameroon, Egypt, Mauritius, Sirra Leone, Uganda, Afrika Kusini, Nigeria na Zimbabwe.
Lakini pia timu za Uingereza, Malaysia, Taiwan, Iraq na India zilionesha nia ya kuja kama waalikwa ingawa ushiriki wao utategemea maamuzi ya bodi ya Kabaddi Afrika (Africa Kabaddi Federation na World Kabaddi).
Mashindano hayo yameahirishwa huku kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ya mchezo huo kilichoteuliwa na Kamati ya Ufundi kikiwa mbioni kuingia kambini ili kuanza rasmi maandalizi ya mashindano hayo chini ya makocha kutoka nje ya nchi kwa kusaidiana na wa hapa ndani.
Kilichochelewesha timu hiyo kuanza kambi ambayo awali ilipangwa kuanza rasmi Novemba Mosi ni kusubiri kuwasili kwa makocha wa kimataifa wa mchezo huo kutoka nchini India, Amrik Singh na Vijender Singh ambao walitarajiwa kutua hapa nchini kabla ya Novemba 15 kwa ajili ya kuanza kuinoa timu hizo.
Rais wa Chama cha Mchezo cha Kabaddi Tanzania (TKSA) Abbdallah Nyoni ameuambia Mtandao huu kuwa, Kamati iliyoandaliwa kwa ajili ya mashindano ya Afrika ya Kabaddi 2020, yaliyopangwa kuanza mwezi ujao sasa yameahirishwa hadi Februari mwakani kutokana na sababu nyingi zilizo nje ya uwezo wao.
Kwa sasa matarajio ya Kamati iliyoandaliwa ni kuwa timu nyingine zitaweza kushiriki katika tarehe hiyo iliyopangwa kutokana na baadhi yao kwa sasa kushindwa kuthibitisha kutokana na kuendelea kukabiliwa na ugonjwa wa Corona.
“Mashindano haya ya Afrika ambayo yangeanza mwezi ujao sasa yatafanyika Februari 17 hadi 21, 2021 na tunatarajia nchi wanachama zitaweza kupata muda zaidi wa kuandaa timu zao ili kufanya mashindano haya kuwa na ushindani wa hali ya juu,” amesema Nyoni.
Licha ya mashindano hayo kuahirisha, wamezitaka nchi wanachama zitakazoshiriki mashindano hayo kuwasilisha majina na nakala za pasipoti za wajumbe wao kabla ya Desemba 31, 2020.
Kusogezwa mbele kwa mashindano hayo pia kutapelekea mabadiliko kadhaa katika kalenda yao ya mashindano ambayo mwezi huu ambapo mbali na kupokea walimu hao pia walitakiwa kufanya tathimini ya maandalizi ya mashindano ya Afrika ikiwa pamoja na kuandaa miundombinu ya mashindano (Hoteli kwa timu, viwanja, chakula na usafiri) pamoja na kufanya semina elekezi kwa wanahabari wa Tanzania juu ya kuripoti mchezo wa kabaddi, sheria na kanuni nyingine.
Desemba 8 na 9, 2020 watapokea timu ya wakaguzi na maafisa wa ufundi pamoja na wanahabari toka nje watakaoambatana na maofisa wakuu wa World Kabaddi, Africa Kabaddi Federation na NKIF na Desemba 10 timu zitaanza kuwasili kwa ajili ya mashindano yatakayoanza tarehe 11 hadi 13.
Desemba 14 timu zilikuwa zinatakiwa kuanza kuondoka hapa nchini huku Desemba 16 na 17 viongozi wangefanya tathmini ya mashindano na kuanda ripoti ambayo ingewasilishwa Desemba 25 na kuvunja Kamati.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025