Na Mwandishi wetu, Timesmajira
MICHUANO ya Lina PG Tour msimu wa tatu imeanza leo kurindima katika Viwanja vya TPC Moshi ambapo zaidi ya wachezaji wa gofu 131 wamejitokeza kushindana.
Mashindano hayo ambayo kwa mara ya kwanza yalifanyika mwaka jana yanaendelea tena mwaka huu yakiwa na lengo la kumuenzi mchezaji gofu wa zamani timu ya Taifa ya wanawake marehemu Lina Nkya ambaye alikuwa na mapenzi makubwa na mchezo huo.
Akizungumza na waandishi wa habari Kiongozi wa mashindano hayo, Ayne Magombe alisema kati ya wachezaji hao waliojiandikisha kushiriki wachezaji wa gofu wa kulipwa na chipukizi ni 59 huku wachezaji wasindikizaji wakiwa 72.
Amesema mashindano hayo yameanza leo na yanatarajiwa kumalizika Juni 1, 2025 na kwamba yanafanyika kila mwaka kwa kujumuisha klabu za wachezajii wote wanaopenda kushiriki mchezo huo kutoka maeneo mbalimbali nchini.
“Mashindano haya yameandaliwa na familia ya Said Nkya katika kumuenzi mama Lina hivyo niwaombe wapenzi wote wa mchezo wa gofu hasa waliopo Moshi na sehemu mbalimbali kujitokeza kushiriki. Kwa pamoja tuongeze ujuzi zaidi, kukuza vipaji na vipato vya wachezaji wetu,” amesema na kuongeza
“Mashindano ya Lina Tour ni endelevu, kwa sasa tuna mashindano matano kwa mwaka, lakini tukipata sapoti kwa wadau wengine tunaweza kuwa na mashindano mengi zaidi ili kukuza huu mchezo,” amesema

Naye mchezaji wa gofu wa kulipwa kutoka klabu ya Gymkhana Dar es Salaam, Fadhil Nkya alisema ameitaka jamii hasa vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki mashindano hayo ambayo yanalenga kuongeza ujuzi na kukuza vipaji.
Hata hivyo Fadhili alisema kila mtu ana uwezo wa kucheza mchezo huo wa gofu na kwamba mishuano hiyo ya Lina inawasaidia wachezaji kufanya mazoezi ya kutosha ili kushiriki mashindano ya kimataifa nje ya nchi.
hivyo ameitaka jamii kuondoa dhana kuwa mchezo huo uchezwa na matajiri.

“Kwa miaka mitano ijayo naiona gofu kuja kuwa kubwa sana na wadau wakijitokeza kutusaidia tunaweza kufanya makubwa, tumeanza mwaka juzi lakini matokeo mazuri yamejitokeza, huu ni msimu wa tatu tunawaomba wadau kujitokeza ili kusapoti hiki kinachofanyika,” amesema Fadhil
Kwa upande wake baadhi ya wachezaji wa kulipwa wa gofu kutoka klabu ya Gymkhana Dar es Salaam wamesema wamejiandaa vizuri kushiriki michuano hiyo na wanaamini wataibuka washindi.
More Stories
Prof.Mbede:Nishati ya umeme wa Sola imepunguza vifo vya wajawazito
Rais Samia apongezwa kuanzisha bima ya afya kwa wote
Serikali yajipanga kudhibiti matumizi yasiyo sahihi kuelekea uchaguzi mkuu