December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbwana Samatta

Mashabiki wa Aston Villa Bongo punguzeni matusi hamjui ya kesho

Na Philemon Muhanuzi, TimesMajira Online

NWANKWO Kanu alipoombwa amuongelee Idion Ighalo aliyekuwa akitakiwa na Manchester United alisema ni mchezaji mwenye nguvu.

Hakuishia hapo akasema yeye kwa uzoefu wake wa kuwa mchezaji miaka ya nyuma anaamini Ighalo atakuwa na mchango katika ushambuliaji.

Kanu alihakikisha anamuongelea vyema sana Mnigeria mwenzake aliyekwenda kuwa raia wa kwanza wa taifa hilo maarufu kuchezea Manchester United.

Wanigeria wameshavuruga timu zote kubwa za Ulaya, kuanzia Inter Milan, Barcelona mpaka Dynamo Moscow ya kule Russia. Wanapofaulu Wanigeria ndipo tunapofeli Watanzania.

Katika suala la mahusiano ya kimataifa, tunapungukiwa ustaarabu. Kupungukiwa ustaarabu kwa upande wetu kulianza kujionyesha baada ya Mbwana Samatta kufanikiwa kununuliwa na Aston Villa.

Akaanza kushambuliwa Jack Grealish kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, kwamba hampi pasi za mwisho Samatta!. Matusi na majibizano ya kijinga yakaanza kuonekana mitandaoni haswa katika kurasa za Aston Villa.

Wazungu wenye timu yao wakajikuta wakiwa na mshangao wakijiuliza, hawa jamaa vipi mbona wanakuwa na michango ya kimaongezi yenye ushamba mwingi!.

Nadhani walikuwa wakitucheka sana baada ya kugundua kuwa Samatta ni mchezaji wetu wa kwanza kuwahi kuchezea klabu ya ligi kuu ya Uingereza.

Nina uhakika hata Samatta mwenyewe kila alipokuwa akiwasha simu yake ya mkononi na kutembelea kurasa za klabu yake atakuwa alijawa na mfadhaiko.

Maoni mengine ni ya kijinga tu, mengine ni ya mtu mgeni wa kuchangia mawazo yenye kulingana na kiwango cha klabu ya ligi ya Uingereza. Samatta katuamsha kwa yeye mwenyewe kupambana mpaka kufika alipofika.

Kwamba tunaweza kuifuatilia ligi kuu ya Uingereza bila ya mchezaji wetu hata mmoja kuonekana kwenye runinga lakini tunapokuwa nae mmoja basi kuna aina fulani ya ustaarabu tunaopaswa kuwa nao.

Ikitokea Ighalo akaonekana hafai tena kuwepo katika kikosi cha Manchester United hatasomeka shabiki Mnigeria akiwatukana makocha wa timu hiyo.

Wanajua kwamba wapo vijana wengine wa Kinigeria kwa maelfu wenye uwezo wa kuja kununuliwa na Manchester United.

Hawana ule ushamba wa kuziwekea nongwa kurasa za klabu kubwa ambayo mshahara inaomlipa mchezaji raia wa nchi yao unagusa maisha ya Wanigeria wanaoishi Nigeria na wengine wa huko huko Uingereza.

Mbwana Samatta wa sasa amepevuka sana kifikra tofauti kabisa na yule aliyetoka Simba na kwenda TP Mazembe.

Anayajua maswali ya mtego ya waandishi wa habari na namna ya kuyajibu. Anajua dhamana ya klabu anayochezea na yapi ni ya kuweka hadharani na yapi sio ya kusikilizwa na wasiohusika.

Anapowaasa mashabiki wanaomfuatilia mitandaoni kwamba waache kuizodoa Aston Villa anakuwa akiongea kama nahodha wa Taifa Stars.

Kwani nahodha ni muongozaji wa wachezaji wakiwa uwanjani na hata nje ya uwanja analo jukumu la kuipa jamii taswira chanya. Ni mwalimu wa maadili kwa mashabiki wote wenye kufuatilia ligi zetu za ndani na za kimataifa.

Anawafikiria kina Kevin John na wadogo zake wengine pale anapowasihi mashabiki wasiendelee na huu utaratibu wa kuikosea heshima Aston Villa mitandaoni.

Na kwa ustaarabu huu wa Samatta ndio anapokumbukwa Kanu anayewaambia wazungu kwamba Ighalo atawafaa na wasimuache.

Tujifunze kumuongelea mtanzania kwa namna ya kumjengea kukubalika na sio kumuongelea kwa namna ya kudhani kuwa tunampenda kumbe ndio tunajiharibia.

Lakini tatizo ni lile lile la kuanza kuucheza mpira wa ushindani awamu ya nne ya Jakaya Kikwete. Tuna kama miaka kumi na nne tu ya kuamka na kuufahamu mpira wa kimataifa upo vipi.

Bado ni miaka michache kulinganisha na mataifa mengi ya Afrika ya Magharibi na Kaskazini. Kujichanganya kimataifa kwa wenzetu ndio maisha yao ya kila siku.

Hawawezi kujisahau na kuanza kuongea lugha zisizo na staha kwenye kurasa za timu kubwa ambazo miaka ijayo zinaweza kuwaona wachezaji wetu na kufikia hatua ya kuwanunua.

%%%%%%%%%%%%%%