Masauni: Serikali inategemea
TADB kukuza kilimo haraka
Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Dar
NAIBU Waziri Wizara wa Fedha na Mipango, Hamad Masauni, amesema Serikali inajivunia ukuaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ambao umeambatana na ongezeko la utoaji mikopo nafuu.
Ameahidi Serikali kuendelea kutegemea benki hiyo katika kukuza kilimo nchini.
Akizungumza baada ya kutembelea makao makuu ya benki hiyo jijini hapa, Masauni, amesema kwamba Sekta ya kilimo imepewa umuhimu mahususi katika mpango wa tatu wa maendeleo ya miaka mitano na kwamba Serikali itaendelea kuitegemea benki katika kukuza sekta ya kilimo, na kueleza kwamba Serikali inafurahishwa na namna benki inavyotoa mikopo kwa wakulima.
“Kwa dhati kabisa niseme nimefurahishwa na kasi ya utoajia wenu wa mikopo tangu kuanzishwa kwa benki hii, kutoka sh. bilioni 30 hadi kufikia sh. bilioni 300.
Hili ni jambo la kujivunia na liwe chachu kwenye utendaji wenu na kuhakikisha mikopo inapatikana na kutolewa kwa wakati,” amesema Masauni.
Ameipongeza benki kwa jitihada inayofanya kuinua wakulima wadogo na kueleza kwamba Serikali inaiangalia sekta ya kilimo kwa jicho la pekee katika mpango wa maendeleo ya miaka mitano.
“Nyinyi ni wadau namba moja katika utekelezaji wa mpango huu. Hamna budi kuendelea kushiriki kikamilifu katika kutekeleza azma hii ya Serikali,” ameeleza.
Amesema kuwa pamoja na kutoa mikopo, benki pia itoea elimu juu ya faida ya upelekaji fedha katika sekta ya kilimo na faida za utoaji wa mikopo nafuu kwa waombaji.
Amesema benki ikifanya hivyo, juhudi hiyo itachochea wananchi wengi kuwekeza katika sekta hiyo ambayo amesema kwa kiasi kikubwa ndiyo inayozalisha malighafi kwa viwanda vya Tanzania.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB, Ishmael Andulile Kasekwa, amemshukuru Waziri Masauni kwa kutembelea makao makuu ya benki na kujionea mwenyewe hali halisi na amemhakikishia kwamba benki itaendelea kufanya kazi zake kwa kufuata taratibu na miongozo iliyowekwa wakati wa uanzishwaji wake.
“Tutatekeleza vyema malengo ya Serikali katika kuianzisha benki hii na kuona inashiriki kikamilifu katika kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo nchini,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine, amemhakikishia waziri kuwa benki itatekeleza majukumu yake kwa weledi ili kuboresha sekta ya kilimo kama serikali inavyotarajia.
“Kwa niaba ya benki nakuhakikishia kuwa tutakuwa mstari wa mbele katia kutekeleza majukumu yetu ili kuleta maendeleo katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi,” ameahidi Bw Justine.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi