Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Hamad Masauni, amezitaka Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) na Benki ya CRDB PLC kuhakikisha ushirikiano wao katika kuendeleza biashara ya kaboni nchini unaleta manufaa ya kiuchumi, kijamii na kimazingira kwa kila Mtanzania.
Masauni ametoa kauli hiyo jijini Antalya, Uturuki, wakati wa hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya NCMC na CRDB Bank, inayolenga kuchochea ukuaji wa soko la kaboni nchini pamoja na kuvutia uwekezaji katika miradi ya kijani.
Amesema biashara ya kaboni inapaswa kuwa na mchango wa moja kwa moja katika kuboresha maisha ya wananchi, kwa kuzingatia upatikanaji wa ajira, uhamishaji wa teknolojia na uwezeshaji wa jamii zinazozunguka maeneo yanayotekelezwa miradi hiyo.

Ameeleza kuwa ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuunganisha utaalamu wa NCMC wa kuratibu na kusimamia biashara ya kaboni na uwezo wa CRDB katika huduma za kifedha na uwekezaji, jambo litakalowezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuanzisha na kutekeleza miradi inayostahili.
Aidha, ameitaka CRDB kuendelea kubuni mifumo na suluhisho bunifu za kifedha zitakazorahisisha upatikanaji wa mitaji kwa waandaji wa miradi ya kaboni na wadau wengine wanaoshiriki katika soko hilo.
Hata hivyo, Masauni amesisitiza kuwa utekelezaji wa miradi ya biashara ya kaboni lazima uzingatie Sheria ya Usimamizi wa Mazingira pamoja na Kanuni za Usimamizi wa Mazingira (Biashara ya Kaboni) za mwaka 2022 na marekebisho yake ya mwaka 2023.

Amesema upatikanaji wa fedha za uwekezaji haupaswi kutafsiriwa kuwa ni kibali cha kuanza kutekeleza mradi bila kufuata taratibu za kisheria na kupata idhini kutoka kwa mamlaka husika.
Amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya kitaasisi na udhibiti ili kuhakikisha biashara ya kaboni nchini inaendeshwa kwa uwazi, uwajibikaji na uadilifu wa kimazingira, huku ikihakikisha manufaa yake yanawafikia wananchi na Taifa kwa ujumla.

More Stories
Rhino Rangers yapewa nguvu ya kupanda Ligi Kuu
Barrick North Mara yazindua Wiki ya Mahusiano.
AFDB kuipatia Tanzania Dola Milioni 26 za Mabadiliko ya Tabianchi