December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Masasi yampa tano Rais Samia

Na Esther Macha,Timesmajira, Online,Masasi

MWENYEKITI Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Mtwara , Julius Kaondo, amesema lengo la Serikali ni kuwezesha kundi la watu wenye changamoto ya kiuchumi katika maeneo yao kwa kuwapa usaidizi ili waweze kujinyanyua wenyewe.

Kaondo amesema hayo juzi wakati wa kikao cha Wazee maarufu na Mkurugenzi wa Mji wa Masasi wanaonufaika na Mpango wa kunusuru Kaya Masikini (TASAF).

Mwenyekiti Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Mtwara , Julius Kaondo,

Amesema lengo la serikali kuja na mpango wa TASAF ni kuwasaidia wanufaika kupunguza umasikini na kuweza kujisimamia kwa kipato kwani Mungu hakutuumba tuwe maskini zingine zinakuja sababu tu ya changamoto za kimaisha.

“Serikali yetu inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikaona iwape misaada na wasaidizi wake ambao ni kama Mkurugenzi wa Mji wa Masasi anaendeleza kwa kuwapenda na kuwaita sasa ndo mnapata kidogo ambacho serikali inakigawa kwenu licha ya kupitia mambo mengi,” amesema .

Mkurugenzi wa Mji wa Masasi Erica Yegella akizungumza na wazee ambao ni wanufaika wa mpango wa TASAF hawapo pichani

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mji wa Masasi mkoani Mtwara, Erica Yegella amesema kuwa lengo la kuwaita wazee hao ni kujitambulisha ili waweze kumfahamu kwa sababu ni Mkurugenzi mgeni katika mji huo.

“Sisi kama serikali tunasimamia TASAF na nyie ndo walengwa lazima tukutane, tuzungumze, tubadilishane mawazo na kupeana ushauri tufanye nini ili tuweze kutoka kwenye umaskini, tutapata taarifa za afya na huduma bora za afya kwenye maeneo yenu mnayoishi kama mtakuwa na changamoto yeyote wakuu wa idara na vitengo vyote wapo, nimekuja kwenu kujitambulisha,“amesema Erica.

Akizungumzia miradi ya visima ya TASAF 19 vyenye thamani ya mil.45 vya mwaka wa fedha uliopita Yegella amesema kuwa ni miradi mizuri na imekamilika zikiwemo barabara za TASAF yenye kilometa moja eneo la Temeke.

Wazee wanufaika wa TASAF

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Masasi ,Cecyl Mwambe amesema kuwa wamekuwa wakipata malalamiko mengi kutoka kwa wanufaika wa mpango wa TASAF kuhusu fedha kuchelewa na wanufaika wengine kupata nusu ya fedha.

Mbunge wa Jimbo la Masasi ,Cecyl Mwambe

Ambapo wamekuwa wakisumbuliwa kwenye mabaraza ya Madiwani hivyo maafisa wanaohusika na TASAF wasaidizi wa Mkurugenzi waweze kuwajibika ipasavyo kupunguza au kuondoa changamoto hiyo sababu kila mtu ana mahitaji.