March 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Masaburi afanya ziara kuhamasisha kujiandikisha daftari la mpiga kura

Na Heri Shaaban, Timesmajira Online,Dar

MBUNGE wa Viti Maalum Wanawake Mkoa Dar es Salaam, Janeth Masaburi, amefanya ziara mkoani humo kwa ajili ya kuwahamasisha Wananchi kushiriki zoezi la kujiandikisha katika maboresho ya Daftari la Mpiga Kura lililoanza Machi 17 hadi 23,mwaka huu.

Masaburi alizindua zoezi la kujiandikisha katika daftari la Mpiga Kura katika eneo lake Kata ya Segerea kituo cha Migombani na baadae kufanya ziara Wilaya ya Ubungo, Kinondoni na Kata ya Buguruni Jimbo la Segerea.

Mbunge Masaburi aliongozana na Viongozi wa Umoja wa Wanawake wa maeneo hayo ambao walipita katika masoko kuonana na makundi maalum ya Mama lishe ,Baba lishe na wananchi.

Hivyo amewataka wananchi wote wakajiandikishe ili waweze kupata fursa ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu,kwani kupiga kura ni haki ya kila mtu lakini lazima uwe umejiandikisha

Amesema kuna watu wamehamia taarifa zao zinatakiwa kurekebishwa na wengine wametimiza umri wa miaka 18 nao wakajiandikishe ili waweze kupata haki ya kupiga kura mwaka huu.