November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Marenga: Kuna vipengele kwenye sheria ya habari vimebeba ukakasi

Na Jackline Martine, TimesMajira Online

IMEELEZWA kuwa Sheria ya Uhalifu wa Mtandaoni iliyotungwa Mwaka 2015, ina adhabu zilizowekwa kwa makosa ambayo hayapo wazi kinyume na Ibara ya 13 (6)(C) ya Katiba ya Jamhuri hivyo inapaswa kufanyiwa mabadiliko.

Hayo ameyasema Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA – TAN) James Marenga, wakati akizungumza na waandishi wa habari za mtandanoni leo tarehe 20 Julai 2022, jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa sheria hiyo imebeba maneno yenye ukakasi hivyo tusipokuwa makini sheria hizo zitaumiza watu wengi zaidi;

“Neno kama ‘kwa namna nyingine ama kusudio na kinyume cha sheria,’ ni maneno hatari yanayotumika hasa kuharamisha jambo ambalo sio kosa kisheria. Maneno haya unaweza kuyaona kuwa ya kawaida, lakini ni hatari sana,” amesema Wakili Marenga.

Pia amesema, sheria hiyo kupitia Kifungu 7 (i)(g) iliyotungwa mwaka 2015, imevuruga uhuru wa faragha ambapo taarifa binafsi za mtu zinaweza kuchukuliwa na polisi kinyume na Ibara ya 16(i) ya Katiba ya Tanzania.

“Sheria hii katika Kifungu cha 50(2)(b) kinaondoa haki ya mtu kukata rufaa kinyume na Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba, lakini pia Kifungu cha 38(2)(b) cha sheria hii kinaruhusu usikilizwaji wa shauri mahakamani hata bila muhusika kuwepo.

“Hukumu ikitolewa, ndio unatafutwa na kufungwa bila kujua kesi yako ilipelekwa mahakani lini, na kwa kosa gani. Ndio maana tunasehma sheria hii inatakiwa kupitiwa upya,” amesema Wakili Marenga.

“Unakamtwa kisha ndio unaoneshwa karatasi ya kesi yako na hapo hapo unapelekwa moja kwa moja jela. Tutunge sheria zenye utu.”

Kwa upande wake, Deodatus Balile ambaye ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), amesema kuna tatizo kwenye sheria hiyo na kwamba, baadhi ya vipengele vinapaswa kuondolewa kabisa.

‘’Sheria inaruhusu kesi yako kuendeshwa bila wewe mwenywe kujua. Kesi unaweza kufunguliwa Mwanza, siku unashuka mtaani unakutwa unapigwa tanganyikajeki.”

“Wanaweza kiufanya hivyo, sheria inaruhusu. Tunapopigania hii sheria iondolewe ama ipitiwe upya, watu wajue tunapigania maslahi ya wengi,’’ amesema Balile.