Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
SERIKALI ya Marekani ina mipango ya kuwadhibiti wanafunzi kutoka nchi za Afrika Mashariki na maeneo mengine duniani katika kuendelea na masomo kwenye vyuo vikuu nchini humo.
Kwa mujibu wa VOA, hatua hiyo itanachukuliwa kwa kuwekwa masharti mapya ya viza, ambayo yatadhibiti ukaazi wao.
Iwapo mapendekezo ya hivi karibuni ya Wizara ya Usalama wa Ndani ya Marekani yatatekelezwa, wanafunzi kutoka nchi nyingi za Afrika, zikiwemo Kenya, Tanzania na Uganda, watazuiliwa kupata viza za kukaa nchini kwa zaidi yamiaka miwili.
Hiyo ina maana kwamba wanafunzi hao wa kigeni ambao watakuwa na nia ya kuhitimu kwa shahada zinazochukua zaidi ya miaka miwili katika vyuo vikuu vya Marekani, hawataweza kufanya hivyo tena.
Kwa mujibu wa utawala wa Rais Donald Trump, mapendekezo hayo yanalenga nchi ambazo zimerekodi zaidi ya asilimia 10 ya wanafunzi ambao wamezidisha muda wao wa kuwa nchini, kinyume na masharti ya viza zao.
Wanafunzi watakaoathiriwa moja kwa moja iwapo hatua hiyo itachukuliwa ni wa kutoka Kenya, Rwanda, Uganda,Tanzania, Burundi, Sudan Kusini, Somalia na Ethiopia.
Wengine ni kutoka Benin, Burkina Faso, Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,Jamhuri ya Congo, Côte d’Ivoire, Djibouti, Equatorial Guinea, Eritrea, Gabon na Gambia.
Mataifa mengine ni Ghana, Guinea, Guinea-Bissau, Liberia, Libya, Malawi, Mali, Mauritania, Niger, Nigeria, North Korea, Papua New Guinea, Senegal, Sierra Leone, Sudan, Togo na Zambia.
Wengine ni kutoka Afghanistan, Bhutan, Guyana, Haiti, Iran, Iraq, Kosovo, Kyrgyzstan, Moldova, Mongolia, Nepal,North Korea, Papua New Guinea, Philippines, Samoa, Syria, Tajikistan, Tonga, Turkmenistan, Tuvalu, Uzbekistan,Vietnam na Yemen.
Kenya inaorodheshwa namba moja kati ya nchi za Afrika Mashariki zilizo na wanafunzi wengi kwenye vyuo vikuu vya Marekani na ni ya tatu kati ya nchi za bara la Afrika zilizo Mashariki mwa jangwa la Sahara kwa idadi kubwa yawanafunzi hao ikifuatiwa na Ethiopia.
Nigeria, ambayo inaongoza kwenye orodha hiyo, ilikuwa imewatuma wanafunzi 13,423 mwaka jana, ambalo ni ongezeko la takriban asilimia sita kutoka kwa kipindi cha kati ya mwaka wa 2017 na 2018. Nchi ya pili kwa wingi wa wanafunzi ni Ghana.
Aidha, ingawa wizara hiyo ilieleza kmuna uwezekano kwa wanafunzi kuomba waongezewe muda wa viza zao baada ya miaka hiyo miwili, hakuna hakikisho kwamba wataongezewa muda huo.
Wakili wa masuala ya uhamiaji, Aaron Reinchlin-Melnick, ambaye pia ni mchambuzi wa sera za uhamiaji katika Baraza la Uhamiaji wa Marekani alinukuliwa na gazeti la The East African akisema kwamba, hatua hiyo itawaathiri wanafunzi wengi na kusababisha wasiwasi kuhusu mstakabali wa elimu yao.
Mapendekeo hayo pia yanazitaka viza za ukazi wa wanafunzi kutoka kwa nchi ambazo zimeorodheshwa kama wadhamini wa ugaidi ikiwemo Sudan, Iran, Syria na Korea Kaskazini kuwa za miaka miwili pekee.
More Stories
Jay-Z aunganishwa na P Diddy kwa kumdhalilisha binti wa miaka 13
Samia avuna makubwa Mikutano ya Uwili G20
Dk. Mpango amwakilisha Samia sherehe za Uhuru wa Lesotho