Na Dady Igogo,Timesmajiraonline,Dar
RUSHWA ni janga kuu linaloitafuna Tanzania kwa kasi ya
kutisha, likikandamiza haki, kutafuna uchumi na kudhalilisha utu na heshima ya mwanadamu.
Tangu enzi za Mwalimu Nyerere na ahadi namba nne ya mwana TANU iliyosema;
“Rushwa ni adui wa haki, sitatoa wala kupokea rushwa” hadi kipindi rushwa ilipovalishwa joho la kuitwa takrima, bado rushwa imeendelea kuwa janga kuu la wazawa.
Enzi hizo ukienda ofisini bila bahasha, utazungushwa! Bahasha ilichukua nafasi ya barua rasmi.
Wakati wananchi walililia shule za kata, wachache walijilimbikizia
mali. Mapambio ya kauli mbiu za rushwa zilizidi kuliko utashi mwema ya kisiasa.
Walioshiba hawakujali waliolala njaa! Rushwa ilipofusha dhamira na macho yao.
Kulikuwa na maumivu makali ya wananchi kutokana na rushwa iliyopigiwa kelele kwa miaka mingi.
Kulikuwa na madhila ya haki kununuliwa mahakamani, mnyonge kukandamizwa, upendeleo wa rushwa huku, ajira za rushwa za ngono ziliendelea kuwa janga kuu la Taifa.
Sote ni mashahidi kuwa rushwa ilisafishwa kwa kupewa majina matamu kama vile takrima, mlungula, pata maji, lete picha. Majina haya yalikua ni tafsida ya kusafisha kichafu kuwa kisafi na halali kuwa haramu.
Kutokana na usugu wa donda la rushwa, Rais Benjamin Mkapa aliunda tume ya Rais ya uchunguzi maaarufu kama Tume ya Warioba.

Tume hii ilikuja na mapendekezo ya kujenga mfumo wa kitaasisi ya kupambana na changamoto ya rushwa.
Naweza kusema, kuwa hatua hii ndiyo ilikua dhamira ya dhati ya Serikali dhidi ya mapambano ya kuzuia na kudhibiti rushwa nchini.
Tume ya Warioba iliainisha sababu za kushamiri kwa rushwa kuwa ni pamoja na mishahara midogo ya watumishi wa umma, ukosefu wa uwajibikaji wa taasisi za umma, ukosefu wa elimu ya uraia na haki za kikatiba, kutokuchuliwa kwa hatua wahusika wa rushwa na kukosekana kwa utashi wa kisiasa.
Katika kufanyia kazi mapendekezo ya ripoti ya Tume ya Warioba, Tanzania ilitekeleza awamu tatu za mkakati wa Taifa dhidi ya rushwa na Mpango wa utekelezaji katika kuendeleza hatua za kuweka mwongozo wa kisera katika kushughulikia masuala ya rushwa na utawala bora nchini.
Hadi sasa, awamu tatu za Mkakati zimetekelezwa: awamu ya I: 2001 – 2005, awamu ya II: 2006 – 2011; na awamu ya III: 2017 – 2022 na sasa awamu ya IV: 2023-2030.
Pamoja na kuwa rushwa ni changamoto ya kidunia ambapo kwa nchi
zinazoendelea linachochewa na umaskini uliokithiri, ujinga na mmomonyoko wa kimaadili, ni ukweli usiokua na shaka, kuwa kiwango cha rushwa tangu kuasisiwa kwa mkakati wa mapambano dhidi ya rushwa na mpango wa utekelezaji awamu ya nne kiwango cha rushwa kimepungua tofauti na awali.
Hii leo dunia nzima inakiri kuwa Tanzania inapiga hatua dhidi ya rushwa. Hata hivyo, bado kuna wachache wenye “miwani ya giza.”

Hawaoni hatua hizi. Hatua hizo zimeiwezesha Tanzania kushika nafasi ya pili katika ukanda wa Afrika Mashariki na nafasi ya 14 kwa nchi za Afrika kwenye mapambano dhidi ya rushwa, na hii ni kwa mujibu wa taarifa ya Taasisi ya Transparency International
ya mwaka 2024 ambapo kwenye corruption perception index ilipata alama 41/100.
Alama hii ni alama ya juu kufikiwa na Tanzania tangu mwaka 2012. Hili nalo hawaoni?
Hadi kufikia 2025, Serikali imefanikiwa kudhibiti na kuokoa kiasi cha Shilingi bilioni 211.95 na kuzirejesha Serikalini kupitia operesheni mbalimbali za uchunguzi wa tuhuma za rushwa.

Kiasi hicho cha fedha kilikua kimepigwa’ na watu. Fedha hizi zilizookolewa zinaweza kujenga idadi ya madarasa ya shule
10,550.
Sambamba na hilo Serikali ya Rais Samia imetaifisha mali zenye thamani ya Shilingi bilioni 35.688 zikijumuisha nyumba, viwanja, magari pamojna na fedha taslimu Shilingi bilioni 1.17. Hii ni hatua kubwa sana kuelekea katika mapambano ya kudhibiti rushwa.
Ni dhahiri, kuwa bado kuna changamoto kubwa, lakini hatua fulani yenye kufurahisha imeweza kufikiwa.
Ijulikane kuwa rushwa ni janga la dunia. Kwa mujibu wa Mfuko wa Mo Ibrahim, Afrika inapoteza takribani dola bilioni 128 za Kimarekani kila mwaka kutokana na vitendo vya rushwa, sawa na asilimia 50 ya mapato yake ya kodi na asilimia 25 ya pato la Taifa.
Uimara wa kusimamia manunuzi na hesabu za Serikali kwenye mashirika ya kiserikali, taasisi, tawala za Serikali za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na Serikali Kuu zimeendelea kuimarishwa mwaka 2024. Kwa mujibu wa ripoti ya CAG 2024, alitoa jumla ya hati 1,301 katika ya hati hizo, hati zinazoridhisha zilikua hati 1295, sawa na asilimia 99.5 hati zenye shaka zilikua tano sawa na asilimia 0.4, hati mbaya ilikua moja sawa na asilimia 0.1.
Jambo hili limeongeza uimara wa kimfumo na kitaasisi katika matumizi sahihi ya fedha za Serikali tofauti na hapo awali.
Waliowahi kunyonya kupitia zabuni na mikataba feki, lazima watavaa miwani ya mbao wasipate kupongeza hatua ambazo zimechuliwa na Serikali ya Awamu ya Ssita.
Si kwamba rushwa haipo kabisa, bali siyo tena biashara ya wazi kama awali ambapo kutoa kitu kidogo ilikua kama salamu za asubuhi.
-MWISHO-

More Stories
Ukusanyaji wa Taarifa na Hatari za Kutoa Taarifa Binafsi Mtandaoni
Migogoro na uhamishaji janga lakisiasa, kibinadamu barani Afrika
Miaka minne ya mageuzi chini ya Rais Dkt. Samia