Judith Ferdinand na Fresha Kinase, TimesMajira Online, Mara
SERIKALI mkoani Mara kwa kushirikiana na Chemba ya Wafanyabiashara Kilimo na Wenye Viwanda (TCCIA) mkoani humo wanatarajia kufanya maonesho ya biashara ya kimataifa (Mara International Business Expo 2022) kuanzia Septemba 2 -11,2022,.
Maonesho hayo yatawakutanisha wafanyabiashara,kampuni,wakulima, wafugaji na wajasiriamali kutoka ndani ya Mkoa huo na nje ya nchi.
Huku lengo ni kuwezesha kutangaza bidhaa zao pamoja,vivutio mbalimbali na fursa za kiuchumi zilizopo mkoani humo ili ziweze kuwanufaisha wananchi na kuufungua Mkoa wa Mara kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki na kidunia.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mara Dkt. Noel Crispine,akizungumzia na Waandishi wa Habari kuelezea maandaliza ya maonesho hayo katika mkutano uliofanyika ukumbi wa uwekezaji uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara ambapo maonesho hayo yatafanyika katika uwanja wa Kumbukumbu ya Karume Mjini Musoma katika siku hizi zote
Dkt. Crispine amesema kuwa, Mkoa huo umeandaa muongozo unaojumuisha fursa zilizopo ikiwemo sekta ya utalii, kilimo,viwanda kwani umebarikiwa kuwa na fursa ya hifadhi ya Serengeti na Ziwa victoria.
Hivyo kazi ya serikali ni kutafsiri fursa hizo ili ziwaletee wananchi maendeleo na kwamba, sekta binafsi ni muhimu ikashirikishwa kwa upana kuchagiza mafanikio hayo.
Amesema, kupitia maonesho hayo Mkoa unaweza kuinukaa na kufahamika zaidi, hivyo kuwavuta wawekezaji toka sehemu mbalimbali za dunia waje walete mageuzi chanya ya kiuchumi ndani ya Mkoa wa Mara na kuzitumia fursa zilizopo mkoani humo kwa tija.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Kilimo na Wenye Viwanda (TCCIA) Mkoa wa Mara Boniphace Ndengo, amesema maonesho hayo yatawakutanisha washiriki 50,000-100,000 ambalo wanalenga kuufanya Mkoa huo uwe eneo jipya la uwekezaji kwa kuzitangaza fursa mbalimbali za kiuchumi kimataifa.
Ameongeza kuwa, TCCIA Mkoa wa Mara inakusudia kuendelea kushirikiana na wafanyabiashara mbalimbali duniani ili kuwaambia uzuri wa Mkoa huo na kwamba wakiwekeza watapata tija kubwa kiuchumi na kuwanufaisha wanaMara kiuchumi kupitia sekta muhimu za uzalishaji.
“Wafanyabiashara wakubwa tunatarajia baada ya maonesho kutakuwa na makongamano na majukwaa mbalimbali yatafanyika kuja kuonesha jinsi gani Mkoa sasa unaendelea,kupunguza migogoro kati ya wawekezaji na wananchi ili kujenga mahusiano bora na habari kubwa iwe ukuzaji wa biashara na yatajumuisha washiriki 50,000 – 100,000,” amesema Ndengo.
Pia amesema katika maonesho hayo chemba mbalimbali za wwfanyabiashara zimealikwa kutoka Uganda, Kenya, Kongo na Burundi ambapo zimethibitisha kuleta washiriki.
“Balozi mbalimbali tumezialika na Zimbabwe imethibitisha kushiriki wengine tulio waalika ni Balozi Marekani, China, India pia maonesho haya yatashirikisha wadau muhimu mategemeo yetu ni kuzalisha ajira kwa vijana waipende sekta binafsi badala ya kutaka ajira za serikali na kuacha fursa zinazowazunguka bila kuzifanyia kazi,”amesema Ndengo.
Mratibu Mkuu wa Maonesho hayo Benard Mwata amesema kuwa, maonesho hayo yatajumuisha kampuni zaidi ya 200 na wamejipanga vyema kuhakikisha yanakuwa na matokeo chanya.
Naye Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini Vedastus Mathayo amesema kuwa kila mwananchi wa Mkoa wa Mara maonesho hayo yanamhusu, hivyo analojukumu la kuhakikisha anafanya uhamasishaji ili watu wengi waweze kujitokeza kushiriki kuonesha bidhaa zao na kuona fursa mbalimbali.
Mathayo ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Mara kwa kuishirikisha kikamilifu sekta binafsi katika maonesho hayo na kwani ni muhimu katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa nyanja za kijamii na kiuchumi.
More Stories
Maghorofa Kariakoo mikononi mwa Tume
ITA chatakiwa kutoa mafunzo ya viwango vya juu na kasi ya maendeleo ya Kisayansi
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi