January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maofisa Watendaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi

Na Israe Mwaisaka, Timesmajira Online,Nkasi


Maofisa Watendaji wa uboreshaji daftari la kudumu la mpiga kura ngazi ya Kata, wametakiwa kuifanya kazi hiyo kwa weledi kama wanavyoelekezwa na kanuni na sheria ili kuweza kufikia lengo kusudiwa.

Wito huo umetolewa jana na Ofisa Mwandikishaji wa Wilaya ya Nkasi Ladislaus Mzelela, kwenye ufunguzi wa semina ya siku mbili kwa Maofisa Watendaji wa uboreshaji daftari la kudumu la mpiga kura ngazi ya kata,ambapo amedai kuwa weledi ndio utakaowawezesha wao kufanikisha zoezi hilo muhimu kwa taifa .

Amesema, ni jukumu lao muhimu kuona wanavifahamu vikwazo vinavyoweza kufifisha zoezi hilo,kisha wakatafuta ufumbuzi wa haraka kwa lengo la kuona kazi hiyo inafanyika kwa kiwango kinachotakiwa .

Pia amewataka kuzingatia maelekezo ya tume huku akiwasisitiza kuwa Mawakala wa vyama vya siasa watakuwepo kwenye vituo vinapofanuika zoezi hili kwa lengo la kuhimiza wapiga kura kujiandikisha ingawa hawatakiwi kuingilia majukumu yao ya uandikishaji.


Hata hivyo amesisitiza ushirikishwaji wa wadau wote wa uchaguzi katika kufanikisha kazi hiyo,kwani kila mmoja ana umuhimu wake katika kufanikisha zoezi hilo.


Watendaji hao wa uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura ngazi ya kata wamepewa mafunzo mbalimbali ikiwemo ya uraia,ujazaji wa fomu mbalimbali wakati wa zoezi zima la uandikishaji ikiwa ni pamoja na mafunzo ya mfumo wa uandikishaji na vifaa vya BVR Kit.

Zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura linatarajia kuanza Januari 12 na kumalizika Januari 18,2025.