Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
WATAALAMU wa Maendeleo ya Jamii, wametakiwa kuhakikisha wanaelimisha wananchi kuhusu ushiriki wao katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050,huku wakitumia lugha rahisi ambayo itawezesha mwananchi wa chini hususani vijijini kutambua dira hiyo ni nini.

Akizungumza Juni 17,2026 wakati akifungua kongamano na mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii Tanzania(CODEPATA), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana,Dkt. Joel Nanauka,amesema Serikali ipo katika utekekalezaji wa Dira ya 2050,yenye lengo la kujenga taifa jumuishi lenye usawa,haki, mitazamo na fikra chanya.
Hivyo Maofisa Maendeleo ya Jamii wana jukumu muhimu la kuhakikisha jamii inatambua uwezo wao wa kutumia rasilimali zilizowazunguka kujiletea maendeleo pamoja na kubadili fikra,mitazamo,mila na desturi ambazo zinaweza kukwamisha maendeleo.
“Dira ya Taifa 2050 inalenga kujenga jamii yenye fikra chanya, maarifa na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, huku vijana wakipewa nafasi kubwa katika kuleta mabadiliko hayo,”amesema Dkt.Nanauka.
Kwa upande wake Rais wa CODEPATA Victor Kabuje, amesema utekelezaji wa Dira 2050 hauwezi kutegemea miundombinu, uwekezaji katika teknolojia pekee, lazima ujikite pia katika maendeleo ya watu katika jamii.
Ambapo amesisitiza kuwa ili dira hiyo itekelezwe ipasavyo wananchi wanapaswa kuelewa vema wapi tumetoka,wapi tulipo? na wapi tunaenda na mtu pekee wa kuwapa tafsiri rahisi na inayoeleweka kirahisi ni Mtaalamu wa Maendeleo ya Jamii.

Hivyo Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii wana weledi na mbinu ya kuiwezesha jamii kufikia malengo ya dira hiyo ambayo yanahimiza Tanzania tuitakayo 2050 kwa kuwa na Watanzania wenye elimu bora na ujuzi unaoendana na teknolojia na uchumi wa kisasa.
Jamii yenye afya njema,kipato kizuri na maisha yenye ustawi huku umaskini ukipungua kwa kiwango kikubwa,pia jamii yenye ajira zenye tija na staha au biashara zinazozalisha mapato ya kutosha,inayoishi katika mazingira salama na amani yenye miundombinu bora na huduma za kisasa.Pia yenye usawa wa fursa bila kujali jinsia,umri au kabila na yenye uwezo wa kushiriki katika maendeleo ya taifa na kunufaika na rasilimali za nchi.
“Ili kufikia adhima ya Dira 2050, Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii ni kiungo baina ya Serikali na Wananchi,kwani wanaendelea kutoa mchango kuhakikisha mafanikio hayo yanaonekana kupitia uwezeshaji wa jamii kunufaika na huduma zinazotolewa na Serikali na wadau kupitia sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, kilimo, mifugo, uvuvi, maji, mazingira, miundombinu, nishati, ustawi wa jamii, uwezeshaji wa wanawake na vijana kiuchumi pamoja na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia,”amesema Kabuje.




More Stories
DCP Ngoso, DCF Ngenya na DCI Mwaifuge wajionea huduma Magerezani
VETA yathibitisha uwezo kwa mhitimu mlemavu
TANTRADE yafungua fursa za Biashara kati ya Tanzania,Urusi