Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
MAOFISA waandikishaji 60 wa Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii iliyoboreshwa (ICHF) wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mkoani Mwanza, wamepatiwa mafunzo ya namna ya kutumia mfumo mpya wa malipo kwa njia ya kielektroniki kwa kutumia namba ya kumbukumbu(control number).
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, John Wanga amewataka kufanya kazi ya uandikishaji kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu kwani hatarajii kusikia Ofisa Mwandikishaji anachukua fedha na kuziweka mfukoni.
Amesema, lengo la mpango huo ni kuwafanya wananchi wapate huduma bora wakati wote iwapo wana pesa au hawana pesa huku pia akiwasisitiza hata wao ni vyema wakajiunga na bima hiyo kwani ni nzuri.
Pia amewataka maofisa wasimamizi ambao ni maofisa maendeleo ya jamii kuhakikisha wanaelimisha jamii ili iweze kuona na kutambua umuhimu wa bima hii ili wananchi waweze kupata huduma hiyo kwa urahisi.
Kwa upande wake Ofisa Maendeleo ya Jamii ambaye pia ni Mratibu wa ICHF Manispaa ya Ilemela, Leonard Robert amesema, ICHF katika Manispaa hiyo wanatarajia kuanza kutumia mfumo mpya wa malipo wa kielektroniki ambapo mwanachama atapatiwa namba ya kumbukumbu (control number) kwa ajili ya kufanya malipo.
“Lengo la mfumo huu mpya ni kupunguza na kuondoa kabisa upotevu wa fedha uliokuwa ukitokea katika mfumo wa malipo ya zamani na kurahisisha ulipaji kwa mwanachama hivyo tutahakikisha kila kitu kinakwenda sana ili kuwawezesha wananchi waliojiunga kupata huduma bora, ” amesema Robert.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu