Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
HALMASHAURI ya Manispaa Tabora imefanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa kero ya upatikanaji huduma za afya kwa wakazi wa mjini na vijijni ikiwemo kuboreshwa miundombinu ya elimu katika shule zote hivyo kufanikisha utekelezaji ilani ya uchaguzi kwa asilimia 100.
Hayo yamebainishwa juzi na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Seif Salum alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisi kwake ambapo alisema miradi yote imetekelezwa kwa ufanisi mkubwa hivyo kuwezesha wananchi kunufaika.
Amesema kwa mwaka jana na mwaka huu wa fedha wamepokea jumla ya sh bil 41.4 zilizotolewa na serikali ya ya awamu ya 6 chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuboreshwa huduma za jamii katika sekta hizo.
Amebainisha kuwa fedha hizo zimeleta tija kubwa katika utoaji huduma kuanzia kwa watalaamu na jamii kwa ujumla na kwa upande wa sekta ya elimu zitachochea kiwango cha ufaulu katika shule zote.
Mbali na elimu na afya Kaimu Mkurugenzi ameainisha sekta zingine zilizoboreshwa katika halmashauri hiyo kuwa ni maji, kilimo, miundombinu ya barabara na utawala ambapo wameweza kujenga nyumba bora za watumishi na kutoa usafiri kwa watendaji wa vijiji na kata ili kuwarahisishia usafiri.
Amefafanua zaidi Seif alisema mafanikio hayo yameweza halmashauri kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM kwa asilimia 100 na kuongeza kuwa wataendelea kusimamia ipasavyo fedha zote zinazoletwa na serikali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
‘Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutupatia fedha hizo, pia ametuletea kiasi cha sh bil 6.4 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya afya katika hospitali yetu ya wilaya na tumepata vifaa vya kisasa vya kutolea huduma’, alisema.
Baadhi ya huduma zilizoboreshwa katika hospitali hiyo ni huduma ya mama na mtoto ambapo sasa akinamama wajawazito kutoka katika zahanati na vituo vya afya mbalimbali watapata huduma bora zaidi.
Ametaja huduma nyingine kuwa ni ya mionzi (x-ray na ultra sound), ambayo imepunguza kero ya wananchi kufuata huduma hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Kitete.
Seif ameongeza kuwa pia wamejenga vituo vya afya na zahanati katika kata na vijiji mbalimbali na zingine kuboreshwa miundombinu na zingine ziko katika hatua mbalimbali ya ukamilishaji ili kuwezesha wananchi kupata huduma bora.
Kuhusu miradi ya elimu amemshukuru Rais Samia kwa kuwapatia sh bil 8.2 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya, vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na nyumba za walimu ili kuboresha mazingira ya kusomea watoto.
Aidha ameongeza kuwa walipokea kiasi cha sh bil 17.7 kwa ajili ya uboreshaji miundombinu ya shule kongwe za sekondari za Tabora wavulana, Tabora wasichana, Milambo na Kazima na kubainisha kuwa sasa zina mwonekano wa kisasa.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua