March 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mangariba 130, waweka visu chini Siha


Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, mangariba zaidi ya 130 wa Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro wamekubali kuacha mila hiyo kandamizi na kujiunga katika vikundi vya kujiendeleza kiuchumi.
Mangariba hao wamkubali kuacha mila hiyo baada ya kupewa ujuzi wa kujiendeleza kiuchumi, ambapo kinamama zaidi ya 1300, sasa wamejiunga katika vikundi 51 vya kuwekeza na kufanikiwa kuzalisha kiasi cha 100.7 milioni kwa mwaka.
Msimamizi Mkuu wa Mradi kutoka Taasisi ya Friedrich Naumann Foundation for Freedom, (FNF) Veni Swai amesema mangariba hao waliamua kuacha kukeketa wasichana na wanawake baada ya kupewa mbinu za ujuzi wa kiuchumi.
“Tulijitahidi kuwafundisha madhara yanayotokana na ukeketaji, madhara kama kutokwa damu nyingi, taratibu walianza kuelewa, lakini ilibidi tuwaeleweshe kwa kina na baadaye walikuwa tayari kushirikiana na FNF, kuwa walimu kwa wanawake wengine,” amesema Veni


Anasema FNF waliwafikia mangariba wengi lakini 132 walikubali kushirikiana na FNF na kufikia hatua ya kutoa taarifa polisi au kwa vyombo vya usalama kuzuia kesi za ukeketaji.


“Mangariba walioacha ukeketaji, wanakwenda kwenye sherehe za mwisho wa mwaka za ukeketaji na kujitahidi kutoa elimu kwa familia kuacha ukeketaji,” anasema


Kwa mujibu wa FNF, mangariba hao walikuwa wakibadili mbinu za ukeketaji ili kukwepa mkono wa serikali au wadau wa kupinga ukeketaji na badala yake walianza kukeketa Watoto wachanga.
“Kuna wakati tulipata taarifa kuwa, mwanamke ambaye hajakeketwa akiolewa katika familia ambayo wanakeketwa, na ikatokea,Mwanamke akajifungulia nyumbani, basi mwanamke anakeketwa wakati wa kujifungua,” anasema


Amesema miongoni mwa shughuli za kiuchumi walizozifanya ni kilimo cha mbogamboga, biashara ndogondogo.
“Kubwa tunaloendelea kufanya kama FNF ni kuendelea kuhamasisha watu wenye ushawishi kwenye jamii kama hizi, kama wazee wa kimila, kusaidi kupaza sauti ili kumaliza ukeketaji,” amesema
Veni amesema baadhi ya vijiji vilifikia hatua ya kutunga sheria ndogondogo za kuzuia ukeketaji katika maeneo yao ambazo kimsingi zimesaidia watu kuogopa kutekeleza mila hizo kandamizi.
Amesema mradi huu umefanyika kata ya Donyoranyi na Karansi, lakini bado FNF tuna mpango wa kufanya kampeni ya kumaliza ukeketaji katika kata za Jirani.
Wanawake hao wa jamii ya kimasai, wanaeleza mafanikio ya kupewa elimu ya kiuchumi, ambayo yanawawezesha kutatua changamoto za kifedha.
Evaline Laitayo anasema

“Nimeweka maji nyumbani kwangu, Watoto wangu wanakwenda shule nawalipia mimi mwenyewe, nikiona sina hela naenda kukopa kwenye kikundi,” anasema
Mwaka 2021, wasichana 240 kati ya 600 wa shule za msingi na sekondari wilaya ya Siga, waliripotiwa kufanyiwa ukeketaji wakati wa likizo. Lakini kufikia mwaka 2024, ni wasichana 20 tu ndio waliofanyiwa ukeketaji.
Veni ameongeza:

“Tunapoadhimisha Siku hii, ujumbe upo wazi, kuhimiza mabadiliko, na jamii, asasi za kiraia na serikali zinapoungana, tutaunda jamii isiyokuwa na ukeketaji”
Mmoja wa wanawake waliopewa elimu wilaya ya Siha, Janeth Lukumay amesema vikundi hivyo vimewawezesha kuacha kutegemea ukeketaji kama kipato.
“Nimetoka kwenye maangamizi nimekwenda kwenye mwanga, nimekataa ukeketaji kabisa,” amesema Janeth
Amesema wanawake, wanaume nao wamepata elimu na kuacha ukeketaji, Joseph Kivuyo, amesema wanaume wanapotumia nguvu familia inakosa amani.“Ningewaomba kinababa, washirikiane na kinamama, tupinge ukeketaji, tumeshajitambua kuwa mtoto wa kike akipata elimu anamkumbuka baba na nyumbani kwao kwanza,” amesema Kivuyo.