January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mamilioni ya mbung’o dume yahasiwa nchini

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Kibaha

WAKALA wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kupitia kituo chake kilichopo Tanga imehasi mamilioni ya mbung’o dume kwa lengo la kutokomeza mbung’o hao kuendelea kuzaliana.

Hatua hiyo inalenga kuzuia ugonjwa ya malale (kwa binadamu) na nagona (kwa mifugo), unaenezwa na vimelea vinavyoitwa ndorobo kutoka kwa mbung’o.

Hayo yalisemwa juzi wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani na Mtendaji Mkuu wa TVLA, Dkt. Furaha Mramba wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari waliotembelea Taasisi ya Chanjo Kibaha (TVI) pamoja na kujionea uzalishaji wa chanjo ya mifugo unaofanywa na taasisi hiyo.

Alisema tangu waanze kuhasi mamilioni ya mbung’o dume, kiwango cha kuzaliana kwa mbung’o kimepungua na kwa upande wa Zanzibar wamefanikiwa kuwatokomeza kabisa.

Kwa mujibu wa Dkt. Mramba, wakishahasi mbung’o dume kazi inayofanyika kituo cha Tanga, hupeleka madume hayo maeneo wanakopatikana mbung’o kwani hata wakipanda majike wanakuwa hawana uwezo wa kuwazalisha.

Wataalam wa Taasisi ya Chanjo Kibaha (TVI) wakiandaa chanjo kwa ajili ya mifugo

“Kwa hiyo tunachokifanya kwenye kituo chetu cha Tanga ni kuzalisha mamilioni ya madume ya mbung’o na kuwahasi na kisha kuwapeleka walipo wenzao, ambapo wanakuwa wastani wa madume tisa waliohasiwa kwa jike mmoja,” alisema Dkt. Furaha na kufafanua kwamba kati ya mbung,o dume kumi kwa jike moja, tisa wanakuwa wamehasiwa, hivyo huyo mmoja hawezi kufanya chochote kwani anazidiwa na hao madume waliohasiwa.

Alizidi kufafanua kwamba kiwango cha mbung’o kuendelea kuzaliana kimepungua kwa kiwango kikubwa na watafika hatua watawatokomeza kabisa.

Mbung,o ni nini?

Mbung’o ni mdudu jamii ya inzi ana miguu sita kila upande mitatu. Ana mabawa kama ilivyo nzi chakula chake ni damu.

Muonekano wa mbung’o ni mdogo kiasi akiwa na ukubwa zaidi ya inzi na anauma wanyama na binadamu. Mbung’o wanapatikana Kusini mwa Jangwa la sahara,kama Vile Tanzania, Burundi, Rwanda na Zanzibar (sasa wametokomezwa)

ng’ombe aliyekufa kwa ugonjwa wa nagana unaoenezwa na mbung,o

Nihatari kwa kueneza ugonjwa wa malale kwa binadamu ambapo mtu anakuwa anasinzia sinzia. Ugonjwa huu unaenezwa na mbung’o, huku kwa wanyama wanyama kama ng’ombe unaitwa nagana.