Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
KAMATI ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza,imeazimia mambo manane ya kuhamasisha jamii umuhimu wa amani na ushirikiano, ili kujenga mazingira salama kwa kila mwananchi.
Kaimu Mwenyekiti Mwenza wa Kamati hiyo, Mchungaji Dk.Jacob Mutash, amesema hayo Septemba 21, mwaka huu, baada ya majadiliano ya kina yaliyohusisha viongozi wa dini wa kamati hiyo ya amani ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani.
Akisoma maazimio hayo Mchungaji,Dk.Mutash, amesema wanalaani vikali vitendo vya ukatili, mauaji, kutekwa na kutoweka kwa watu.Kwani vitendo hivyo vinachafua taswira ya nchi, kuleta hofu na taharuki katika jamii.
“Jukumu letu ni kushughulikia viashiria vya uvunjifu wa amani kabla ya matatizo kutokea,hivyo siku ya Amani Duniani hatuwezi kukaa pembeni katika kuhamasisha amani,”amesema Dkt.Mutash.
Amesema, kamati hiyo inawasihi viongozi wenzao wa dini na jamii, kukemea vitendo vya ukatili na mauaji yanayotokea nchini,huku akisisitiza kuwa ni lazima kila mmoja achukue jukumu la kulinda amani na usalama.Ambapo ameeleza kuwa hatua hiyo itajenga msingi wa jamii yenye umoja na maendeleo.
Pia imewahimiza Watanzania kukataa na kukemea vitendo vya rushwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa, na kuhimiza umuhimu wa kuchagua viongozi bora watakaoweza kuleta maendeleo endelevu katika jamii.
“Ni muhimu viongozi wa dini,kukemea na kulaani matukio hayo na hatua zinazohitajika ni pamoja na ushirikiano kati ya serikali na mashirika mengine,kutafuta ufumbuzi wa matatizo haya kwani serikali inahitaji ushirikiano wa kuimarisha amani,”amesema Dkt.Mutash.
Kamati hiyo ya viongozi wa dini imeshauri serikali kwa uwezo wake itumie vyombo vya usalama kuchukua hatua za haraka kukabiliana na changamoto hizo.Pia kuimarisha usalama wa wananchi, visikatishwe tamaa kwa kauli zisizo za msingi,viendelee kusaidia juhudi za kudhibiti mauaji,ukatili na matukio ya uvunjifu wa amani.
Hata hivyo,imewaaasa vijana kujiepusha na mihemko inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani, huku ikisisitiza wananchi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, kuanzia Oktoba 11 hadi 20 mwaka huu pia washiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Viongozi wenzetu wa dini,msiwe na upande wowote wa itikadi za kisiasa,wabaki kuwa washauri na walezi kwa jamii,katika nyumba za ibada tuweke ratiba ya kuombea nchi amani na viongozi wake badala ya kusubiri miongozo ya serikali,hivyo mambo hayo manane yachukuliwe ndiyo,”amesema Dk.Mutash.
Naye Mwenyekiti Mwenza,Sheikh wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Hasani Kabeke, amesema kamati hiyo ina jukumu la kutetea amani,hivyo ametoa wito kwa serikali,viongozi wa vyama vya siasa, na waandishi wa habari kuhakikisha wanailinda amani ya nchi kwa vitendo.
Ameonya wanaojichukulia sheria mkononi, na wanaolishutumu Jeshi la Polisi lenye jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zao, kuwa huo ni uvunjifu wa amani unaotishia utulivu.
“Hatupaswi kutengeneza mpasuko kati ya jamii na Jeshi la Polisi.Tumekutana,tuzungumze na kuiasa jamii, jukumu la kuilinda na kuitetea amani kama lilivyo azimio la Umoja wa Mataifa (UN),”amesema Sheikh Kabeke.
“Ni fursa muhimu kwa kila mmoja kuleta mabadiliko chanya katika jamii, kuifanya nchi yetu na dunia amani itamalaki,”amesema Sheikh Kabeke.
Mjumbe wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Mwanza,Saada Abass, amesema Watanzania waendelee kudumisha amani.
“Ombi langu kamati ifanye tathmini ya kipi imefanya na wapi haijafikia malengo,pia kizazi cha sasa hakina maadili sababu wazazi wamejikita kutafuta fedha na kuwaacha watoto wajilee wenyewe.Ili kukinusuru, wazazi wawafundishe waliyofundwa na wazazi wao, na wakifanya hivyo matukio haya ya ukatili na mauaji hayatakuwepo,”amesema Saada.
Naye Mchungaji Canon Gershon Yoboka wa Kanisa la Anglikan,ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuomba na kuwaasa kuwa makini na kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani kwani matukio hayo yanakosesha taifa utulivu.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja