Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza umuhimu wa Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira kuwa na takwimu na tathmini zinazoonesha uhalisia wa uchafuzi wa mazingira unaotokana na shughuli za binadamu
Hayo ameyazungumza wakati alipokutana na viongozi na watumishi Waandamizi wa Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), katika kikao kilichofanyika leo kwenye ukumbi wa mikutano wa Kambarage Jijini Dodoma.
Katika kikao hicho ambacho ni mwendelezo wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayofanyika kila mwaka Juni 5,Makamu wa Rais amezungumzia tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kipindi cha miaka mitano tangu aingie madarakani.
“Lengo ni kuona tunaposherehekea Siku ya Mazingira Duniani, Ofisi imekuwa ikisimamia vipi suala zima la uratibu wa udhibiti wa uchafuzi wa mazingira ili kuhakikisha rasilimali zilizopo zinatumika kwa uendelevu.
“Kwa mfano, usimamizi wa miradi ya maendeleo inayolenga kurekebisha mifumo ikolojia na bioanuai, kupunguza gesijoto na kuhakikisha tunapanda miti ili kunyonya hewa ukaa, kupunguza ukame na kuhakikisha usalama wa chakula, kurekebisha mazingira katika migodi kwa kuhakikisha uoto wa asili unarejeshwa mara baada ya migodi hiyo kufungwa,” alisema.
Aidha,alisisitiza umuhimu wa Ofisi kuwa na takwimu na tathmini zinazoonesha uhalisia wa uchafuzi wa mazingira unaotokana na shughuli za binadamu. Kwa mfano; ukataji wa miti kiholela, uchimbaji wa mchanga na vifusi, utiririshaji wa maji sumu na maji taka kutoka kwenye migodi kwenda kwenye vyanzo vya maji, mito na maziwa.
Vilevile ameelekeza kuwa, ili kuweza kuratibu kwa ufanisi shughuli za binadamu zinazochangia kwenye uharibifu wa mazingira kuna umuhimu wa kufanya mapitio ya Sera ya Mazingira ili kuja na mkakati utakaoainisha majukumu, changamoto na maono ya Ofisi kwa kushirikiana na sekta mbalimbali.
Ili kuhakikisha kuwa wananchi wanawajibika moja kwa moja katika utunzaji na usimamizi wa mazingira,alisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa kushirikisha Viongozi wa Serikali za Mitaa ili kuhakikisha kuwa takwimu za mazingira katika sekta mbalimbali zinawekwa sawa kuanzia ngazi za chini.
Pia amepongeza hatua zilizochukuliwa na Ofisi katika usimamizi wa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki.Pia aliagiza Ofisi kwa kushirikiana na TAMISEMI kukamilisha mchakato wa kupatikana na kupewa mafunzo stahiki Wakaguzi wa Mazingira katika Halmashauri zote nchini.
Pia amesisitiza suala la kufanya tathmini katika maeneo yote ya migodi na wachimbaji wadogo ili kubaini kiwango cha uharibifu wa mazingira na kuchukua hatua stahiki na kwa wakati kabla madhara kwa binadamu na mazingira hayajatokea.
Amewataka viongozi na watumishi kuendelea kutoa elimu zaidi kwa umma ili kuongeza uelewa kwa wananchi katika masuala ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira.
More Stories
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme