Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online.
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, imefanya operesheni maalum wilayani Same, mkoani Kilimanjaro kwa siku saba kuanzia Machi 19 hadi 25, mwaka huu ya kusaka biashara haramu ya bangi.
Katika operesheni hiyo,hekali 285.5 za mashamba ya mirungi zimeteketezwa na watuhumiwa saba kukamatwa, akiwemo kinara wa biashara haramu ya mirungi nchini aliyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu, Interindwa Kirumbi, maarufu kwa jina la “Mama Dangote”.

Akizungumza baada ya operesheni hiyo, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema kuwa, Mama Dangote ni mzalishaji na msambazaji mkubwa wa dawa za kulevya aina ya mirungi nchini kwa zaidi ya miaka 30.
Ambaye amekuwa akiendesha mitandao ya biashara haramu ya mirungi na kusimamia masoko ya dawa hizo za kulevya katika maeneo mbalimbali nchini, licha ya kujua kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
Lyimo amesema , mwaka juzi Mamlaka ilifanya operesheni wilayani humo ambapo waliteketeza hekali 535 pamoja na kutoa elimu kwa wananchi ili waachane na kilimo cha mirungi na badala yake wajikite katika kilimo cha mazao mbadala pamoja na ufugaji.
Pia ameeleza pamoja na jitihada hizo, uongozi wa Wilaya ya Same na Wizara ya Kilimo na ya Mifugo waliwapelekea wananchi wa maeneo hayo miradi ya ufugaji wa nguruwe na kugawa miche ya kahawa, iliki na mazao mengine.
Kutokana na juhudi hizo, wananchi wengi wameachana na kilimo na mirungi na kuanza kulima mazao mbadala, japo wapo wachache waliokaidi na kuendelea na kilimo na biashara ya mirungi.
Hata hivyo amesisitiza kwamba mamlaka itaendelea kufanya operesheni kuhakikisha wananchi wote wanaojihusisha na biashara ya mirungi wanakamatwa na hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yao.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha tunatokomeza biashara na matumizi ya mirungi hapa nchini hasa ikizingatiwa kuwa, eneo hili la Same ni kitovu cha uzalishaji,hivyo inayohatarisha ustawi wa taifa letu ndio maana tunafanya operesheni hizi endelevu nchi nzima, kuhakikisha tunadhibiti uzalishaji,usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya shambani na viwandani,”.
Kwa upande wake Agness Mshana, Mtendaji wa Kata ya Ekondi,amekiri kutambua uwepo wa watu wanaojihusisha na kilimo cha mirungi.
Hivyo kama Serikali wameendelea kutoa elimu juu ya madhara ya mirungi ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kupata mazao mbadala ili kuepukana na kilimo hicho.
“Tumejitahidi kuwaletea mradi wa nguruwe pamoja na miche ya miparachichi na kuwapa elimu ya madhara ya dawa za kulevya,kwa maana mirungi ina madhara mengi yakiwemo kuchanganyikiwa, kupoteza nguvu za kiume, kushindwa kuhudumia familia vizuri, kupata saratani na kadhalika,” ameeleza Agness.

Nao baadhi ya wananchi wa Kata ya Tae wilayani Same, akiwemo aliyetambuliks kwa jina moja la Hawa, amesema kuwa, hajui sababu ya watu kuendelea kujihusisha na kilimo cha mirungi kwani kuna mazao mengi yanayostawi kama vile vitunguu, karoti na iliki pamoja na miradi ya nguruwe iliyoletwa na Serikali.
Aidha, ameiomba Serikali kuimarisha miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji wa mazao yanayozalishwa kupelekwa sokoni, hali itakayosaidia wananchi kuwa na uhakika wa masoko ya mazao yao na hivyo kuachana na biashara ya mirungi.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za wazalishaji, wasambazaji, na watumiaji wa dawa za kulevya ili kutokomeza biashara hiyo na kulinda ustawi wa jamii.
More Stories
The Desk and Chair yatoa vifaa saidizi kwa Masatu na mkewe
jengo la mama,mtoto la bilioni 6.5 lazinduliwa Mbulu
Dkt.Malasusa ataka hospitali ya Haydom kuombea wafadhili wanaoishika mkono