June 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makumbusho ya Taifa yatakiwa kuhifadhi kazi za Andanenga(Sauti ya kiza)

Na Bakari Lulela, Timesmajira Online,Dar

SERIKALI  imeitaka Makumbusho ya Taifa kuhifadhi tuzo na kumbukumbu za Sudi Amiri Andanenga (sauti ya kiza) mtaalamu wa fasihi ya kiswahili na mshairi mahiri Tanzania na duniani kote.

Akizungumza jijini Dar-es-Salaam, kwenye hafla maalumu ya kumbukizi za mshairi huyo Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Songoro Mnyonge,amesema kutokana na umahiri wa Andanenga, Makumbusho ya Taifa kuhifadhi tuzo zake mbalimbali na mambo kadhaa ambayo aliwahi kuyafanya katika uhai wake.

“Mzee huyu alikuwa mwanafasihi mkubwa katika ukuzaji wa Lugha adhimu ya kiswahili na ushairi,hivyo tunamkumbuka kwa weledi wa umahiri wake na tunamuenzi kwa falsafa yake ya kukinadi  kiswahili  barani Afrika na duniani kote,” amesema Songoro. 

Songoro amesema,kutokana na umuhimu wa Andanenga pia familia yake iweze kuangaliwa kipekee kutokana na mchango mkubwa aliouonesha ndugu, baba yao ya kukitunza na kukiendeleza kiswahili barani Afrika.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Kulua Kihidija,amesema, Andanenga alikuwa mtu mbobezi hivyo tumepoteza hazina kubwa katika jamii ya kitanzania.

“Wataalamu kama hawa hatunabudi kuwaenzi na kuwakumbuka,kutokana na kuacha alama muhimu ndani ya jamii yetu,kukikomboa kiswahili kutoka katika mikono ya wakoloni na kuwa maalumu hapa nchini kwetu,”.

Mtunzi wa vitabu na rafiki kipenzi wa Mshairi huyo,Chars Mloka,amesema kuwa Andanenga alikuwa mbobezi na mahiri toka enzi za ukoloni hadi kifo chake.Pia alikuwa anapenda kujielimisha kila siku huku akisisitiza kuwe na utamaduni wa kujisomea vitabu kwa kumuenzi gwiji huyo (sauti ya kiza).

Nae mwanafunzi wake Jumanne Shaibu (undi) amesema tukio Hilo ni zito kama alivyokuwa mwenyewe hivyo ameshukuru mwitiko wa watu mbalimbali kuanzia kwenye kutembelea kaburi lake Hadi kwenye hafla hiyo iliyokuwa katika ukumbi wa meya ya Kinondoni Dar es salaam.

Nae Bi  Sikudhani Jalala aliyepatiwa jina la Simba jike na marehemu Andanenga amesema anamkumbuka kwa kumfunza namna bora ya utungaji wa mashairi yenye manufaa na tungo bobevu.