March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makongoro azindua jengo jipya la TCB

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online, Rukwa

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere, ameipongeza Benki ya Biashara Tanzania (TCB) kwa kuendelea kuimarisha huduma za kifedha nchini, wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la benki hiyo Sumbawanga.

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa jengo hilo iliyofanyika Julai 10, 2025,Makongoro amesema kuwa uzinduzi wa jengo hilo ni ushahidi wa dhamira ya benki hiyo katika kusaidia maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi, hasa wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa, wanawake na vijana hususani waishio vijijini.

“Tukio hili la kihistoria linaashiria mafanikio ya benki hii, na hatua muhimu kuelekea ujumuishi wa huduma za kifedha, ukuaji wa uchumi, na maendeleo ya Taifa,”amesema Makongoro.

Mkuu huyo wa mkoa ameishukuru TCB kwa kuguswa na changamoto za kijamii mkoani Rukwa kwa kusaidia sekta za elimu na afya, akisisitiza kuwa huo ni mfano wa taasisi inayowekeza katika ustawi wa jamii.

Kwa upande wake,Ofisa Mtendaji Mkuu wa TCB, Adam Mihayo, amewahakikishia wananchi kuwa benki hiyo itaendelea kutoa huduma bora na bunifu ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiuchumi na teknolojia nchini.

Ameeleza kuwa benki imetenga kiasi cha shilingi bilioni 20 kwa ajili ya kuwakopesha wajasiriamali.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wafanyakazi wa TCB na wananchi wa Sumbawanga waliokuwa na hamasa kubwa kushuhudia tukio hilo la kihistoria.