June 14, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makongoro aielekeza Halmashauri ya Nkasi hoja za kufanyiwa kazi haraka

*Aipongeza Nkasi kwa kupata hati safi

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Rukwa

MKUU wa Mkoa Rukwa Charles Makongoro Nyerere, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kupata hati safi Ikiwa ni kielelezo cha ushirikiano kati ya watendaji ,madiwani na wadau wengine.

Huku akisisitiza baadhi ya hoja ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi haraka kuwa ni pamoja na mwenendo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa mwaka 2023/24,usimamizi wa manunuzi,miradi ya maendeleo,rasilimali watu,mali za halmashauri,matumizi ,upimaji,utekelezaji wa mpango na bajeti.

Akizungumza kwenye kikao maalumu cha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo,kuhusu utekelezaji wa hoja za ukaguzi na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2023-24,Makongoro amesema,msimu uliopita kulikua na hoja nyingi za ukaguzi lakini sasa zimepungua hivyo kuna kitu kinafanyika ndani ya halmashauri.

Amefurahishwa na namna Halmashauri imejishughulisha na ufutaji wa hoja mbalimbali zilizojitokeza,huku akitolea mfano kuwa kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Aprili 2025, Halmashauri ya Wilaya Nkasi,imeonesha kuwa na hoja za miaka ya nyuma 21.

Hivyo kufanya kuwa na hoja 38 na maagizo 4 yenye vipengele 10 ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC) ambapo maagizo mengi yapo katika ya utekelezaji na hoja nyingi kufutwa.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Msalika Makungu, amekiri kuwepo kwa mabadiliko ya kiutendaji katika Halmashauri ya Wilaya Nkasi na kupata hati safi ilistahili kwa namna walivyoamua kushirikiana kwa pamoja.

Amesema,siri ya mafanikio mahala popote pa kazi ni ushirikiano na kufuata kanuni za kiutendaji,kuwa na malengo ya pamoja katika kuyafikia mafanikio waliyoyalenga.

Mkuu wa wilaya Nkasi Peter Lijualikali,amesema ushirikiano uliofanywa na Madiwani na watendaji wa halmashauri hiyo ndio siri ya mafanikio.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Pankrasi Maliyatabu, amesema Madiwani wanamaliza msimu wao wa kiuongozi mwaka huu huku wakiiacha halmashauri ikiwa katika mazingira mazuri na salama katika kutoa huduma kwa wananchi.