November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makinda ahimiza matumizi Bora ya matokeo ya sensa 2022

Na Raphael Okello, Timesmajira Online,
Mwanza

Kamisaa wa Sensa ya watu na makazi 2022 Taifa, Anne Makinda amewaasa waandishi wa habari kuchakata takwimu za matokeo ya sensa uliofanyika mwaka Jana ili waweza kuzitumia kwa usahihi katika kutoa taarifa zitakazochochea maendeleo ya nchi

Makinda amesema hayo Septemba 25,2023 katika mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari kutoka mikoa ya Mara,Mwanza na Kagera yanayohusu usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 yanayofanyika jijini Mwanza.

Kamisaa wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 Anne Makinda, akizungumza katika mafunzo hayo

Amesema waandishi wa habari wanafanyakazi kubwa ya kuhabarisha jamii hivyo ni vyema wapate uelewa mpana juu ya matokeo ya sensa ya 2022 kama dira kamili ya mipango ya maendeleo ya jamii katika ngazi zote.

“Matokeo haya ya sensa ya mwaka 2022 zikitumiwa vizuri na watunga sera kuanzia ngazi za halmashauri zetu yatawawezesha kuleta mipango ya maendeleo yenye tija Kwa wananchi,”amesema Makinda.

Amewataka watafiti kutoka vyuo vikuu mbalimbali, mashirika kutoka nje na ndani ya nchi na taasisi zinginezo kufanya tafiti zao nchini kwa kuzingatia matokeo hayo ya sensa 2022.

Kwa mujibu wa Makinda amesema matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 yamezingatia vigezo vya kimataifa na kwamba yakitumika vizuri katika mipango ya maendeleo Tanzania itapiga hatua kubwa ya maendeleo kwa muda mfupi.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi akifungua mafunzo hayo

Awali akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi alilisisitiza matumizi bora ya matokeo ya sensa.

Ambapo amesema sensa imegharimu fedha nyingi za serikali hivyo matokeo yake yalete ufanisi katika mahitaji ya jamii na mazingira yake.

Amewataka waandishi wa habari kutoka kwenye klabu zao za mikoani kushiriki mafunzo hayo Ili kuchangia katika kufikia malengo ya sensa kama ilivyotarajiwa badala ya takwimu hizo kubaki kwenye makabrasha ofisini.

Kamisaa wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 Anne Makinda wa tatu kushoto huku wa tatu kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa iliyofanyika mwaka 2022

Mafunzo hayo ambayo yanaendelea kwa waandishi wa habari kote nchini yameandaliwa na ofisi ya Taifa ya takwimu(NBS).