Mwandishi Wetu.TimesMajira Online, Mwanza.
BENKI ya NMB imewaalika wakandarasi wa ndani na nje ya nchi wenye mikataba ya ujenzi wa miradi ya miundombinu inayotekelezwa nchini kwenda kukopa bila kulazimika kuweka dhamana ya mikopo hiyo.
Wito huo umetolewa na Afisa mtendaji mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka eneo la Feli mkoani Mwanza hadi Isaka mkoani Shinyanga.
Amesema, mikopo hiyo ni sehemu ya benki hiyo kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya maendeleo na malengo ya Taifa kiuchumi na kijamii.
“Tumeshirikiana na makampuni ya kigeni yanayoratibu miradi mikubwa kama ujenzi wa barabara, pamoja na miundo mbinu ya maji, mpaka sasa tumetoa dhamana ya zaidi ya shilingi bilioni 200, kwenye mradi wa reli ya kisasa (SGR). NMB imefanikisha zabuni kwa makandarasi wazawa zaidi ya 500 katika ngazi ya wilaya na mikoa,” amesema Zaipuna.
Zaipuna alisema, NMB imewezesha manunuzi ya nje ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Mamlaka ya Bandari (TPA) na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kwa kutumia Letters of Credit zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 120.
“Tayari tumetoa dhamana ya Sh. bilioni 48 kwa kampuni za wazawa zinazotekeleza miradi ya umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini, REA,” amesema Afisa Mtendaji Mkuu huyo.
Pamoja na huduma za kifedha, benki ya NMB pia inashirikiana na Serikali kupitia Shirika la Reli nchini (TRC) kulipa fidia kwa wananchi ambao maeneo yao yanapitiwa na miradi ya ujenzi wa reli.
Benki hiyo pia inatekeleza kampeni ya elimu kwa umma kuhusu masuala ya kifedha kwa lengo la kupanua wigo wa ujumuishaji wa kifedha (financial inclusion) kwa makundi yote ya kijamii mijini na vijijini.
Benki ya NMB yenye mtandao wa matawi zaidi ya 226 zaidi ya asilimia 95 wilaya zote nchini, ikihudumia zaidi milioni nne imeongoza sekta ya kibenki kwa faida kubwa nchini Tanzania kwa zaidi ya miaka 10 mfululizo, huku ikitambuliwa kama benki salama zaidi nchini na jarida la Global Finance kwa mwaka 2020. Benki hiyo pia imeorodheshwa katika soko la hisa la Dar es Salaam tangu mwaka 2008.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi