Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline
MAKANDARASI wameaswa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zote zinazoongoza shughuli za ujenzi hapa nchini ikiwemo kulipa ada za mwaka za usajili, kusajili miradi ya ujenzi ikiwa ni takwa la kisheria, kuzingatia usalama wa maeneo ya kazi, nk.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya Mipango na Udhibiti wa Miradi ya Ujenzi (Construction Planning, Organisation and Control) yanayofanyika kwa siku tatu jijini Dar es salaam, Msajili Msaidizi wa CRB, Mhandisi.David Jere,amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kukuza ujuzi kwa makandarasi katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi kuanzia mipango mizuri, mbinu za utekelezaji na mambo yote yanayowezesha mradi kutekelezwa kwa ufanisi.
“Kupitia mafunzo haya mtajifunza misingi ya kuzingatia unapopanga kutekeleza mradi wa ujenzi, ikiwemo kutambua uzito wa kazi husika, malengo ya utekelezaji ili kukamilisha katika muda uliopangwa, kutambua rasilimali zinazohitajika katika utekelezaji wa miradi, upatikanaji wake, mpangilio katika eneo la kazi na usimamizi wa kazi husika pamoja na mada nyingine nyingi kama itakavyowasilishwa na mwezeshaji”, alisema Mhandisi. Jere.
“Sambamba na hayo mtajifunza misingi na mbinu za utekelezaji wa miradi, ikiwemo mawasiliano, utunzaji wa kumbukumbu na namna ya kukabiliana na matatizo yanayojitokeza katika maeneo ya utekelezaji wa miradi pamoja na masuala ya afya na usalama katika maeneo ya utekelezaji wa mradi” aliongeza Mhandisi Jere.
Pia alisisitiza umuhimu wa Makandarasi kuzingatia kutimiza wajibu katika mikataba wanayofunga na waajiri kulingana na makubaliano husika.
“Naomba niwatahadharishe kwamba ukiukaji wa mkataba kwa kushindwa kutimiza wajibu wako, pamoja na hatua zilizoainishwa na mkataba husika, Bodi ikipata taarifa na kuthibitisha kwamba Mkandarasi alikiuka makubaliano, itatoa adhabu kwa mujibu wa sheria, mfano kutelekeza mradi (abandoning the site) ni kosa ambalo likithibitishwa, mkandarasi anafutiwa usajili”,amesema Mhandisi Jere.
Aidha, Pili Wambura, mshiriki wa mafunzo hayo alisema changamoto wanazokutana nazo wakati wa kutekeleza majukumu ya usimamizi wa miradi umempa msukumo wa kushiriki kwenye mafunzo na matarajio yake ni kuimarika vyema katika kusimamia mipango na udhibiti wa miradi ya ujenzi.
“Tumekuwa tunaingia gharama zilizopo nje ya mipango katika usimamizi wa miradi tunayoifanya, hii ni kutokana na usimamizi mbaya, lakini kupitia mafunzo haya naamini tutakwenda kuongeza ujuzi, hali itakayotupa uwezo zaidi katika kusimamia vyema kila mradi tunaopata katika ubora unaostahili na utakaotupa manufaa kwenye kampuni zetu”amesema Wambura.
Sambamba na hilo Wambura aliishukuru Bodi ya Usajili wa Makandarasi kwa kuendesha mafunzo hayo na kutoa rai kwa Makandarasi wengine kuhudhuria mafunzo kila watakaposikia yametangazwa.
Kwa upande wake Mkandarasi Joseph Mataluma alisema ana matumaini kuwa kupitia mafunzo hayo atajifunza vyema namna mkandarasi anavyotakiwa kuusimamia mradi kuanzia hatua za mwanzo hadi kukamilika ukiwa kwenye ubora na viwango vinavyohitajika.
Katika miradi hii ya ujenzi, mkandarasi anatakiwa kuwa na nidhamu ya hali ya juu wakati wa kutekeleza miradi na kufuata taratibu zote zilizopo kwenye mikataba na nyaraka za zabuni. Kwa kufanya hivyo itasaidia kufanyika na kukamika kwa miradi katika ubora unaohitajika”amesema Mataluma.
Mafunzo haya yamewakutanisha washiriki zaidi ya 140 kutoka mikoa mbali mbali hapa nchini.
More Stories
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais
NIDA yawakumbusha wananchi kuchukua vitambulisho vyao