Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
MAKAMU wa Rais Deogratius Ndejembi, ameshuhudia uzinduzi wa Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Benki ya CRDB, ukiwa na lengo la kuongeza kasi ya wananchi kupata huduma ya umeme nchini.
Ndejembi ameshuhudia uzinduzi wa mpango huo leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, unaotekelezwa chini ya kaulimbiu “Kila Nyumba Itawaka – Tumekufikia, Tutakulipia na Utalipa Kidogo Kidogo,” akisema ushirikiano huo ni mfano wa namna Serikali na sekta binafsi zinavyoweza kuunganisha nguvu na rasilimali katika kutatua changamoto zinazowagusa wananchi moja kwa moja.
Kupitia mpango huo, wananchi wa maeneo ya vijijini watawezeshwa kuunganishiwa umeme kwa kupata ruzuku ya Shilingi 27,000 kwa kila kaya kutoka CRDB, ambayo si mkopo. Kwa upande wa wananchi wa maeneo ya mijini, watapata fursa ya kuunganishiwa umeme kwa mkopo kuanzia Shilingi 320,000 wenye riba nafuu.

Ndejembi amesema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mission 300, inayolenga kuongeza kasi ya upatikanaji wa umeme barani Afrika, huku Tanzania ikiwa na lengo la kuwaunganisha watu milioni 8.5 na huduma ya umeme kati ya mwaka 2025 na 2030, sawa na kuwafikishia huduma hiyo takribani watu milioni 1.7 kwa mwaka.
“Miradi kama hii ni muhimu katika kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa kwa ufanisi. Kupitia makubaliano haya, CRDB imejiwekea lengo la kufikisha huduma ya uunganishaji umeme kwa kaya 500,000 kwa mwaka,” amesema.
Akizungumzia umuhimu wa huduma hiyo, Ndejembi amesema umeme ni msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja, familia na Taifa, akieleza kuwa mtoto anahitaji mwanga ili aweze kusoma, mkulima anahitaji umeme kuongeza thamani ya mazao yake, kijana anahitaji nishati kuwezesha ubunifu na teknolojia, huku mfanyabiashara akihitaji umeme kuongeza tija na kuchangia ukuaji wa uchumi.

“Hakuna Mtanzania anayepaswa kubaki nyuma kwa kukosa huduma ya msingi ya umeme,” amesema.
Aidha, Makamu wa Rais ameiagiza TANESCO kwa kushirikiana na CRDB kufanya tathmini ya matokeo ya mpango huo, kutoa elimu kwa wananchi kuhusu gharama na masharti ya huduma hiyo, pamoja na kuhakikisha utekelezaji unaanza mara moja.

Mpango huo unatekelezwa chini ya kaulimbiu “Kila Nyumba Itawaka – Tumekufikia, Tutakulipia na Utalipa Kidogo Kidogo,” ikisisitiza dhamira ya kuwezesha wananchi kupata huduma ya umeme kwa urahisi na kwa masharti nafuu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela, amesema benki hiyo imetenga kiasi cha shilingi bilioni moja kila mwaka kwa ajili ya mpango huo, ambapo kwa kushirikiana na TANESCO itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kutumia fursa hiyo muhimu katika kusukuma mbele maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema kupitia makubaliano hayo, awamu ya kwanza inalenga maeneo ya vijijini, ambapo Benki ya CRDB itawezesha kiasi cha shilingi 27,000 kwa kila kaya inayostahili. Fedha hizo zitalipwa moja kwa moja kwa TANESCO kama gharama za uunganishaji wa umeme, bila mwananchi kuwa na wajibu wa kuzirejesha.
Amesema kwa wananchi wa mijini na pembezoni mwa miji, CRDB itawezesha upatikanaji wa fedha kupitia mikopo nafuu, ambao utalipwa kwa utaratibu utakaowekwa na benki hiyo.
“Mpaka sasa TANESCO ina takribani wateja milioni 6.4, lakini kupitia mpango huu wa ushirikiano tunatarajia idadi ya wateja itaongezeka na kufikia lengo la kuunganisha kaya milioni 1.7 kwa mwaka,” amesema Bw. Twange.

More Stories
GF yakabidhi magari kwa wachimbaji, yaongeza huduma
Homera ampongeza Rais Samia upatikanaji wa Umeme
DIB yasisitiza umuhimu wa Bima ya Amana