October 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DIB yasisitiza umuhimu wa Bima ya Amana

Na Joyce Kasiki, Geita

WANANCHI wanaoweka fedha katika benki na taasisi za fedha zilizopewa leseni wanaweza kulindwa dhidi ya hasara iwapo taasisi hizo zitashindwa kuendelea na shughuli zake, kupitia mfumo wa Bima ya Amana.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Fedha na Uhasibu wa Bodi  ya Bima ya Amana (DIB) Romuli Mtui wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonyesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini katika viwanja vya Dkt.Samia Suluhu Hassan mkoani Geita.

Mtui amewataka wananchi kutumia huduma rasmi za fedha badala ya kuhifadhi fedha majumbani, ikieleza kuwa hatua hiyo inawaweka katika hatari ya kupoteza mali zao na pia kuzuia fedha kushiriki kikamilifu katika mzunguko wa uchumi.

Amesema wananchi wanaofungua akaunti katika taasisi zilizopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hunufaika na Bima ya Amana bila kulipa ada wala kujisajili.

Amesema Bima ya Amana inatofautiana na bima nyingine kwa kuwa mteja halazimiki kulipa mchango wa kila mwaka wala kufanya usajili maalumu ili kunufaika nayo.

“Wananchi wamezoea kwamba kupata bima wanahitaji kujisajili na kuchangia kiasi fulani kila mwaka. Lakini Bima ya Amana ni tofauti kwa sababu mwananchi hakatiwi kuchangia chochote wala hatakiwi kujisajili,” amesema Mtui

Kwa mujibu wa Mtui  , fedha zinazohifadhiwa nyumbani hazishiriki kikamilifu katika mzunguko wa uchumi, tofauti na fedha zilizowekwa katika taasisi za fedha ambazo zinaweza kutumika kutoa mikopo kwa shughuli mbalimbali za maendeleo.

Amesema pia kuhifadhi fedha nyingi nyumbani kunaweza kuhatarisha usalama wa mali hizo kutokana na uwezekano wa kuibwa au kuharibika kwa sababu ya majanga kama moto na mafuriko.

Amefafanua kuwa Mfuko wa Bima ya Amana ulianzishwa mwaka 1999 kwa mtaji wa Serikali wa takribani Sh1.05 bilioni na umeendelea kuimarishwa kupitia michango ya benki na taasisi za fedha wanachama.

Amesema kwa mujibu wa Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, taasisi hizo zinatakiwa kuchangia katika mfuko huo, ambao fedha zake huongezwa kupitia uwekezaji katika hati fungani za Serikali na vitega uchumi vingine.

Aidha, amesema DIB hushiriki katika hatua za kushughulikia changamoto zinazolikabili benki au taasisi ya fedha kabla ya kufikia hatua ya kushindwa kuendelea na shughuli zake.

Amesema ushiriki huo unalenga kulinda maslahi ya wawekaji na kupunguza athari kwa Mfuko wa Bima ya Amana endapo taasisi itashindwa kuendelea na shughuli zake.