August 21, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makame awakalia kooni Ma-DC,utitiri vituo vya ukaguzi

Na Moses Ng’wat, Songwe.

MKUU wa Mkoa wa Songwe, Jabir Omari Makame, amewataka Wakuu wa Wilaya kusimamia kwa karibu utekelezaji wa agizo la kuondoa vituo vya ukaguzi barabarani visivyo na ulazima, akisema utitiri wa vituo hivyo katika umbali mfupi umekuwa kero kwa wafanyabiashara na wananchi.

Makame alitoa maelekezo hayo jana, Agosti 20, 2026, wakati akizungumza katika Jukwaa la Songwe Dira 2050 Forum lililofanyika kwa siku mbili mkoani Songwe, lililolenga kujadili ushirikishwaji wa wadau katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Alisema licha ya agizo la kuondoa vituo visivyo vya lazima kutolewa, baadhi yake bado vinaendelea kuwepo, hali inayolazimu Wakuu wa Wilaya kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa na maeneo yao yanaondokana na vituo visivyo na msingi.

“Haiwezekani w
Wilaya moja inakuwa na vituo vingi vya ukaguzi kwa umbali mfupi, hii kero imekuwa ikilalamikiwa mara kwa mara, hivyo Wakuu wa Wilaya simamieni utekelezaji wa maelekezo haya,” alisema.

Katika hatua nyingine, Makame alilitaka Jeshi la Polisi kupunguza vituo vya ukaguzi visivyo vya lazima, akisema utitiri wa vituo hivyo unaongeza usumbufu na kuchelewesha safari.

Alisema kupunguza vituo hivyo hakumaanishi kuondoa ukaguzi barabarani, bali kuufanya kuwa wa ufanisi kwa kubaki na vituo vinavyohitajika kwa ajili ya usalama na udhibiti, bila kuweka vikwazo visivyo vya lazima kwa wasafirishaji.

Makame alisema kupunguza vikwazo vya aina hiyo ni muhimu katika kuboresha mazingira ya biashara, usafirishaji na uwekezaji, ambayo ni maeneo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Alisema Dira 2050 inahitaji mazingira yatakayowezesha wananchi na sekta binafsi kufanya shughuli za kiuchumi kwa ufanisi, hivyo Serikali katika ngazi zote inapaswa kutambua na kuondoa changamoto zinazoweza kuwa kikwazo kwa biashara na uwekezaji.

Mkuu huyo wa Mkoa alisisitiza kuwa utekelezaji wa Dira 2050 unapaswa kuonekana kupitia hatua zinazoboresha mazingira ya biashara, usafirishaji na huduma kwa wananchi, badala ya kubaki katika mijadala na mipango pekee.

Awali ndani ya jukwaa hilo, wadau mbalimbali walilalamikia kuwepo usumbufu mkubwa kwenye ukaguzi hasa Malori katika barabara Kuu ya Tanzania na Zambia (Tanzam) na kusababisha usumbufu na malalamiko mengi.