Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online Dar
KATIBU wa NEC, Siasa,Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, CPA Amos Makalla, amemtaka Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar-es-Salaam, Zaituni Hamza, kufuatilia mwenendo mbovu unaolalamikiwa na wananchi katika hospitali ya Nguvu Kazi, iliyopo Chanika jijini humo.
Kufuatia malalamiko yaliyotolewa na wananchi walio hudhuria katika mkutano wa hadhara wa Katibu huyo , uliofanyika katika uwanja vya shule ya sekondari Chanika, wameilalamikia hospitali hiyo kuwatoza fedha wajawazito pindi wanapofika kupatiwa huduma ikiwemo kujifungua pamoja na watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanapopatiwa huduma ya matibabu.
Baadhi ya wananchi hao, ambao hawakutana majina yao kuchapishwa kwenye vyombo vya habari, wamesema zipo kero nyingi ikiwa pamoja na uwepo wa watendaji wasiyo kuwa na maadili katika hospitali ya Nguvu Kazi.
“Pale tunapatiwa huduma mbaya labda mpaka utoe chochote kitu, wajawazito tunatozwa fedha pindi tunapoenda kupata huduma ya kliniki, pia hata ukienda kujifungua ukitaka kuhudumiwa haraka na vizuri ni lazima utoe fedha, lakini pia watoto wetu wenye umri chini ya miaka mitano hawatibiwi bure hadi utoe fedha,”amesema mmoja wa wananchi hao.
Pia, wameilalamikia hospitali hiyo kuwa na mfumo mbovu wa uchomaji taka, hali inayowasababishia wakazi wa maeneo ya jirani kuathirika kiafya kutokana na moshi unatokana na taka hizo.
Wakati akisikiliza na kutatua kero hizo, Makalla amemtaka Mganga Mkuu katika Halmashauri hiyo kufuatilia jambo hilo kwa haraka, huku akieleza kuwa Chama cha Mapinduzi kitaendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kero za wananchi zinapatiwa majibu.
“Dhima ya CCM ni kutatua kero za wananchi na si kuzikimbia, hivyo nitoe wito kwa watendaji wote serikalini kutimiza wajibu wenu katika kutoa huduma nzuri kwa wananchi na kufanya hivyo ndiyo silaha ya chama,naomba DMO kesho ufike kwenye hiyo hospitali na kufuatilia malalamiko yote na kuyafanyia kazi,” amesema Makalla.
Aidha, Makalla amewahakikishia Wakazi wa Jimbo la Ukonga kuwa katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, chama hicho kitawasimamisha wagombea wanaokubalika na wenye kiu ya kutatua changamoto za wananchi na si vinginevyo.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba