Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
KATIBU wa Halmashauri Kuu (NEC),Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Amos Makalla ameahidi kufanya siasa za hoja na ustaarabu kwa kuzingatia falsafa ya 4R ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.
Amesema atashirikiana na viongozi wa ngazi mbalimbali za chama na Serikali,kuhakikisha imani ya Watanzania kwa Chama Cha Mapinduzi inaendelea kukua na kukifanya kiendelee kushika dola.
Makalla ametoa kauli hiyo jijini Mwanza Aprili 6,2024 alipohutubia mkutano wa hadhara uliofanyika nje ya Ofisi ya CCM Mkoa wa Mwanza na kuhudhuriwa na wananchi na wana CCM waliojitokeza kumpokea.
Amesema baada ya kurudishwa nyumbani katika kazi anayoipenda,hatofanya siasa za vioja,ataitetea na kuitangaza CCM,kunadi sera,kuyatangaza mazuri iliyoyafanya ya kuwaletea wananchi maendeleo huku akiwataka mabalozi kujipanga kwa uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Lengo la chama chochote cha siasa ni kushika dola,hakuna chama kinahubiri watu kwenda mbinguni,hivyo mabalozi wajipange kwenda katika uchaguzi wa serikali za mitaa,CCM ishinde kwa kishindo pia 2025 ishinde tena kwa kishindo,” amesema Makalla.
Pia katika nafasi za uongozi wa serikali za mitaa wateuliwe wagombea wanaokubalika,viongozi watoe michango ya kukisaidia chama kupata wagombea wazuri wenye sifa na uwezo wa kuwatumikia wananchi.
“CCM tumerudi chini kwa wananchi,kuongea na mabalozi wanaowashikilia wanachama wetu na katika matawi waliko, tutawafuata huko waliko,tutazunguka nchi nzima kuweka mkakati wa ushindi na tukipata ushindi wa kishindo utapeleka ujumbe kuwa Rais Dk.Samia atashinda kwa kishindo na msingi huo ni sasa,”amesema Makalla.
Pia amewataka viongozi wa chama hicho kuelewa majukumu yao, waende kwa wananchi waamini CCM ni kimbilio lao kwa kuwa wanafahamu ndiyo yenye serikali,wathibitishie hayo.
“Tutoe miongozo kwa serikali kutatua changamoto na kero,tuwasikilize na kuwapa matumaini,tukifanya hayo tutakuwa tumefanikisha matumaini ya wananchi hao na kuwandaa kwa uchaguzi,”ameeleza na kuongeza kuwa
“Tunao mtaji wa hoja za kuwaambia wananchi lakini wako watu watapita na kuwaambia barabara hii na zahanati hii haijajengwa na serikali ya CCM,lazima kazi hiyo tuifanye, sisi tusiishie kukagua miradi tu,lazima watu waelezwe wafahamu kazi iliyofanywa na CCM na serikali yake,”.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba