March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makala: GovESB ,Mfumo wa Kisasa wa Kubadilishana Taarifa Serikalini ,Kuchochea uwajibikaji

Na Joyce Kasiki

KATIKA harakati za kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), imepiga hatua kubwa kwa kubuni na kutekeleza Mfumo wa Kubadilishana Taarifa Serikalini, ujulikanao kama Government Enterprise Service Bus (GovESB).

Mfumo huu ulizinduliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa , katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika Juni 23, 2025, katika Viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.

Historia ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA)

Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ni taasisi ya umma iliyoanzishwa kwa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019 ikiwa na jukumu la kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za utekelezaji wa Serikali Mtandao. Hii ni muendelezo wa kazi iliyokuwa ikifanywa na Wakala ya Serikali Mtandao (iliyoundwa mwaka 2012) na hata kabla ya hapo, Idara ya Usimamizi wa Mifumo (DMIS) iliyokuwa chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Lengo kuu la kuanzishwa kwa e-GA ni kuhakikisha taasisi za umma zinafuata Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo katika ujenzi na uendeshaji wa mifumo ya TEHAMA, ili kukuza uwazi, uwajibikaji na utoaji bora wa huduma kwa umma.

Kusanifiwa kwa Mfumo wa GovESB

Kuanzia mwaka 2021, e-GA ilianza kuandaa na kutekeleza mpango wa kujenga mfumo wa kitaifa wa kubadilishana taarifa kwa njia ya kidijitali miongoni mwa taasisi za umma. Lengo likiwa ni kuondoa changamoto ya mifumo ya Serikali kutokuingiliana (interoperability) na kushindwa kusomana kutokana na tofauti katika viwango vya kiteknolojia.

Mkurugenzi Mkuu wa e-GA, Mhandisi Benedict Ndomba, alieleza kuwa GovESB ni matokeo ya utafiti wa kina na kazi kubwa ya kitaalamu iliyolenga kujenga suluhisho la kudumu la mawasiliano baina ya mifumo mbalimbali ya taasisi za umma. Mfumo huu unawezesha mifumo ya zamani na mpya kuwasiliana na kubadilishana taarifa kwa usalama, ufanisi na kwa wakati halisi.

Uzinduzi Rasmi wa Mfumo

Katika hotuba yake wakati wa uzinduzi, Waziri Mkuu Majaliwa aliagiza taasisi zote za umma ambazo bado hazijajiunga na GovESB kuhakikisha zimejiunga kufikia Julai 30, 2025, bila kujali bajeti wala gharama, kwa kuwa mfumo huo hauna ada kwa taasisi. Alisisitiza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu matumizi sahihi ya TEHAMA katika maendeleo ya Taifa.

Waziri Mkuu alieleza kuwa hadi kufikia Juni 2025, ni taasisi 185 pekee zenye mifumo 223 ndizo zilikuwa zimeunganishwa kwenye GovESB, na kuonya kuwa idadi hiyo ni ndogo ukilinganisha na taasisi zote za umma nchini.

Faida za Mfumo wa GovESB

GovESB umebuniwa kwa madhumuni ya kuimarisha muwasiliano ya ndani ya Serikali na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi. Baadhi ya faida zake kuu ni:

Kuboresha utoaji wa huduma kwa wakati kwa wananchi na wadau wengine;

Kuokoa muda na gharama katika uendeshaji wa shughuli serikalini;

Kupunguza makosa ya kibinadamu na kucheleweshwa kwa taarifa;

Kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika utendaji wa taasisi za umma;

Kuwezesha mifumo yote ya umma kusomana (interoperability) bila kujali teknolojia iliyotumika kuijenga;

Kupambana na vitendo vya rushwa kupitia mfumo wa taarifa uliounganishwa.

Waziri Majaliwa alisisitiza kuwa mfumo huu ni nyenzo muhimu ya Serikali katika kuleta mabadiliko ya kweli katika utoaji wa huduma za umma na kupambana na changamoto zinazotokana na urasimu wa kiutendaji.

Hatua za Utekelezaji na Matarajio

e-GA imepewa jukumu la kuhakikisha kuwa mifumo yote iliyounganishwa inaendelea kufanya kazi kwa ufanisi na taarifa zinabadilishwa kikamilifu. Mamlaka hiyo pia inatarajia kuwa taasisi zaidi za umma zitaunganishwa kabla ya mwisho wa mwaka huu, ikiwa ni utekelezaji wa maono ya Rais Samia ya “Serikali Mtandao yenye uwazi, tija na majibu ya haraka kwa wananchi.”

Uzinduzi wa mfumo wa GovESB ni hatua muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea Serikali ya Kidijitali. Kwa kutumia mfumo huu, Serikali imeweka msingi imara wa kuhakikisha kuwa taasisi zote za umma zinashirikiana kwa karibu, kubadilishana taarifa kwa wakati na kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Ni jukumu la kila taasisi ya umma kutekeleza agizo hili kwa bidii na weledi, kwa kuwa mafanikio ya Taifa letu katika zama hizi za kidijitali yanategemea utekelezaji thabiti wa mifumo ya TEHAMA kama GovESB.

-Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa jyckasiki@gmail.com