Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
KATIBU wa Halmashauri Kuu (NEC),Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa,Amos Makalla,leo (jana) amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Said Mtanda,kumfuatilia mkandarasi wa mradi wa ujenzi wa jengo la abiria na upanuzi wa uwanja wa ndege ili ikamilike ndani ya muda.
Makalla ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa Katibu wa NEC,alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa miezi kumi,ametoa maagizo hayo wakati akimkabidhi ofisi Mtanda ambaye kabla ya uteuzi huo mpya alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Akizungumza kabla ya makabidhiano hayo,Makalla amesema Mwanza ni Mkoa wa pili nyuma ya Dar es Salaam kwa idadi ya watu na mchango wa pato la taifa,wananchi wake wanahitaji maendeleo hivyo anaondoka akiwashukuru kwa upendo na ushirikiano waliompatia.
“Nilitoka nje ya ofisi kutatua changamoto na kero za wananchi,nilipata ushirikiano wa kufanya kazi pamoja viongozi wa dini,machifu pamoja na makundi mbalimbali yanataka maendeleo,”amesema Makala.
Makalla amesema alipohamishiwa Mwanza,alipewa maelekezo na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kusimamia miradi ya kimkakati ikamilike na kuleta manufaa na tija kwa wananchi.
Amesema miongoni ni mradi wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza na ujenzi wa jengo la abiria la kisasa lenye hadhi ili kuufanya wa kimataifa,mradi ambao ni kiu ya wananchi wa Mwanza uliokuwa ukisimamiwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa lakini haukuwa na vigezo,ulizua maswali mengi na kuleta changamoto.
“Nilikuta unajengwa kwa Force Account (watalaam wa ndani) kwa sh. bilioni 2.5,ofisi yangu haikuwa na uwezo wa kujenga jengo hilo lenye hadhi ya kimataifa,nilielewa utaniletea matatizo hivyo nikaamua kuurejesha (TAA) Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege,”amesema Makalla.
Amesema uamuzi huo ulisababisha Rais Dk.Samia,akutoa fedha kiasi cha bilioni 28 kujenga jengo la abiria na upanuzi wa uwanja kuhakikisha Mwanza inakuwa kitovu cha usafiri wa ndege,tayari baadhi ya kampuni zimeomba kuutumia uwanja huo.
“Kazi yako kubwa ni kumfuatilia mkandarasi miezi kumi mradi ukamilike ndege zitue tufanye biashara na mataifa mengine,suala la kusafirisha minofu ya samaki isipite Uganda na Kenya,ukarabati wa chumba cha mizigo na mazao mabichi unafanyika,”amesema Makalla.
Pia kukamilika kwa jengo la abiria na upanuzi wa uwanja wa ndege,utakuwa mkakati wa kukuza utalii na ni lazima Mwanza kuwe na mkakati huo ili mtalii akitua,ndani ya saa moja anawaona wanyama Hifadhi ya Serengeti.
“Kipande cha tano cha mradi wa SGR uliogharimu trilioni 3 umefikia asilimia 37, hivyo Bandari ya Dar es Salaam ikichangamka mizigo mingi itakuja Fella,itapita daraja la kihistoria la J.P.Magufuli (Kigongo-Busisi),litaunganishwa na SGR kwenda Congo DRC na Burundi,”amesema Makalla.
Ameeleza kuwa meli ya MV Mwanza imekamilika kwa asilimia 99,kilichobaki ni kuweka samani katika madaraja ya kwanza na la pili na itaanza kazi Mei baada ya kukamilika kwa uboreshaji wa ghati liyakalotumia kutia nanga.
Makalla pia amemkabidhi kitabu cha orodha ya kero na migogoro 427 aliyoisikiliza kimsaidie katika utatuzi na utendaji wake huku akimkumbusha kusimamia tamasha la Bulabo lililompa Uchifu Chifu Hangaya (Rais Dk. Samia) ambalo hufanyika kila mwaka.
Kwa upande wake Mtanda amesema hana hofu na utendaji wake kwani hakuja kuanza upya,hivyo maagizo aliyopewa ya usimamizi wa miradi ya kimkakati ameyapokea na kuahidi kuendeleza akianzia alipoishia.
“Niombe dua na sala,kazi za uongozi ni mgumu sana,sina hofu na utendaji wangu na Mwanza ninyi mpo,uliyonielekeza nimeyapokea,nimekuja kuendeleza ulipoachia siji kuanza upya,uliyoyaamua sitayagusa nitapokea mapya na nisipoelewa jambo viongozi wa CCM mpo na Rais Dk.Samia aliniandaa kabla,”ameeleza Mtandao na kuongeza kuwa
“Mwanza kuna uchumi mkubwa kutokana na idadi ya watu zaidi ya milioni 3,kazi hizi kuna fitina na fitina huongezeka penye riziki,fitina ya kwanza ni fedha na ya pili wanawake na watoto,ili ushinde lazima utengane na fedha,”amesema Mtanda na kuahidi kushirikiana na machifu kufanikisha Tamasha la Bulabo.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam