November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makakala: Tunaanza siku 10 kusaka wahamiaji haramu Loliondo

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Loliondo

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji Dkt. Anna Makakala ametangaza kuanza kwa operesheni maalum ya siku kumi kusaka wahamiaji haramu katika eneo la Loliondo, Ngorongoro mkoani Arusha.

Kamishna Jenerali Makakala amebainisha hayo leo Loliondo, na kusema kuwa zoezi hilo litaenda sawia na zoezi linaloendelea la uwekaji wa alama za mipaka katika Pori Tengefu la Loliondo.

Dkt. Makakala amesisitiza kufuatwa kwa sheria za nchi pale wageni wanapotaka kuingia au kutoka nchini, na kwamba Uhamiaji imejipanga vema kusimamia eneo hilo katika mipaka yote nchini.

“Nchi yetu imebarikiwa kwa kuwa na maeneo mazuri ambayo yanavutia wahamiaji haramu kufika nchini kwa sababu tofauti, hatutakubali hilo litokee wakati wowote ule,” alisema Makakala.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mwalimu Raymond Mangwala amemfahamisha Dkt.Makakala kuwa wilaya yake inaendelea vema na utekelezaji wa zoezi la uwekaji wa alama za mipaka katika eneo la Pori Tengefu la Loliondo na kwamba atatoa ushirikiano katika zoezi la kusaka wahamiaji haramu ili wale wote watakaobainika wachukuliwe hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria za nchi.