January 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makada CCM waungana kumpambania Dkt. Angeline

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

BAADHI ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Ilemela ambao walijitokeza kutia nia ya kuomba ridhaa ya chama hicho kuwapitisha kuwania nafasi ya Ubunge jimboni humo, wamesema watahakikisha wanamuunga mkono mgombea Ubunge wa Jimbo hilo Dkt. Angeline Mabula ambaye amepitishwa na chama kugombea nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Makada hao wamejipanga kupeleka kwa wananchi yale ambayo yamefanyika kwa kipindi cha miaka mitano kwa kila Kata kueleza yale mazuri yaliyofanywa na chama hicho ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Umeme, Reli ya kisasa, Barabara, Maji, Afya, Elimu na kuelezea ilani ya mwaka 2020-25 kuwa CCM inaenda kufanya nini kwa miaka mingine mitano.

Mmoja kati ya waliotia nia 72 waliojitokeza kwenye kinyanganyiro hicho, Cosmas Mwanalinze amesema, kwa msingi mgombea huyo ambaye ameteuliwa na chama na sasa anaendelea na kampeni zake watahakikisha wote wanaungana na kukipa chama chao ushindi ndani ya Jimbo la Ilemela.

“Kama mnavyoona tangu kuanza kampeni kazi tunaifanya jukwaani tunamnadi mgombea wetu, tumefanya hivyo kwenye Kata zote ambazo amepita na bado tunaendelea kumnadi ndani ya Ilemela, tuna fahamu chama chetu kinahitaji ridhaa ya miaka mitano mingine ikiwemo Jimbo letu na maendeleo tunayaona hivyo tunasababu ya kuendelea kumchagua Dkt.Angeline,” amesema Mwanalinze.

Amesema, msingi wa chama chao ni siasa safi na wanawanadi wagombea wao bila kutoa lugha za matusi, na ndio maana wanapeleka sera safi kwa wananchi, kile ambacho wamefanya na kwanini wanahitaji ridhaa tena ya miaka ili waweze kutekeleza yale ambayo hayajatekelezeka.

Kampeni Meneja wa CCM Jimbo la Ilemela Kazungu Idebe, amewaambia wanailemela kuwa wanayosababu kubwa kumchagua Dkt. John Magufuli na wagombea wanaotokana na chama hicho.

Kazungu Idebe

Akizungumza kwa nyakati tofauti katika mikutano mbalimbali ya kumnadi mgombe Ubunge wa chama hicho ambayo imefanyika kwenye baadhi ya kata za Jimbo hilo ikiwemo Nyamanoro, Kahama, Shibula, Pasiansi, Ibungilo, Kawekamo, Nyasaka, Bugongwa, Kirumba, Buswelu na Kitangiri, Idebe amesema katika kipindi cha miaka mitano Dkt. Magufuli kwa kusaidiana na wasaidizi wake akiwemo mgombe Ubunge huyo wamefanya mambo makubwa ambayo nyuma yalishindikana.

Idebe amesema, katika sekta ya afya zahanati zaidi ya 1000 zimejengwa,vituo vya afya zaidi ya 400 na hospitali za Wilaya zaidi ya 90 ikiwemo ya Wilaya ya Ilemela.

Katika kipindi hicho pia kwa Jimbo la Ilemela wamefanikiwa kujenga shule za msingi mpya tatu,sekondari tatu na mbili za kidato cha tano na sita,barabara zimejengwa za kiwango cha lami ambapo awali zilikuwa chini ya km10 lakini Sasa ipo zaidi ya km 30, ikiwemo barabara ya Mjimwema -Isamilo- Big Bite, Sabasaba-Kiseke-Buswelu,maji,barabara,usafiri wa majini umeimarishwa.

Kwa upande wake, Mhandisi Samson Masalu ambaye pia ni mmoja wa watia nia, amewaomba wananchi kuchagua CCM kwa ajili ya maendeleo na kila mmoja ni shahidi kwa yale ambayo yamefanyika,na wao wapo tayari kumuunga mkono mgombea Ubunge huyo ili aweze kushinda pamoja na chama hicho kwa ujumla kishinde kwenye uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.