Na Penina Malundo, TimesMajira Online
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya dereva wa UBER aliyefahamika kwa jina la Joseph Mpokala (51) mkazi wa Mbezi kwa Msuguri .
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,SACP-Lazaro Mambosasa, amesema jeshi hilo lilipata taarifa kutoka kwa mke wa marehemu kuwa mume wake ametoweka tangu Mei 21, mwaka huu huku simu zake zikiwa hazipatikani.
Mambosasa amesema, Mei 26, mwaka huu jeshi hilo lilipopata taarifa hiyo liliaanza msako kupitia kikosi chake cha kupambana na uhalifu.
Amesema, watuhumiwa walioshikiliwa ni pamoja na Godson Mzaura (29) mkazi wa Mbezi Beach, Said Mahadhi (38) Mkazi wa Afrikana, na Denis Urassa (45) mkazi wa Makongo.
“Mei 27 mwaka huu alikamatwa mtuhumiwa Mzaura na kuhojiwa kisha kukiri kufanya mawasiliano na marehemu ambapo alieleza kuwa Mei 21,mwaka huu saa saba mchana walimkodi marehemu ili awapeleke maeneo ya Mbezi na walipofika Mbezi Juu watuhumiwa hao walimuua, Tillya na kumfukia kwenye shimo katika eneo la wazi lenye uzio wa ukuta ambao hujamalizika kujengwa (pagale),” amesema na kuongeza;
“Juni 2, mwaka huu watuhumiwa wote watatu walihojiwa kwa kina na kukiri kuwa walifanya mauaji hayo na kuchukua gari la marehemu namba T 139 DST Toyota IST na kwenda kulificha Kimara Baruti katika nyumba ya wageni ya Api Forest Logde,”amesema.
Aidha, amesema jeshi hilo linakamilisha taratibu za kupeleka jalada kwa mwanasheria wa Serikali na watuhumiwa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
More Stories
Serikali yaja na mwarobaini wa changamoto ya Kivuko Magogoni – Kigamboni
Kisarawe kukata keki ya Birthday ya Rais Samia
Wataalam wa afya wakutana kujadili ugonjwa wa Marburg