December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‘Majukumu ya TAKUKURU yana wigo mpana’

TAASISI ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) ni miongoni mwa taasisi za Serikali zilishiriki kwenye maonesho ya huduma na bidhaa za wajasiriamali kutoka mikoa yote,yaliyofanyika hivi karibuni jijini hapa, kwenye Uwanja wa Nyerere Square.

Kamanda wa TAKUKURU wa Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo, anasema wanatumia kila mbinu kusogeza jamii karibu ili kuielimisha kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu taasisi hiyo.

Lengo kuu lilielezwa naye kuwa ni kuleta ufanisi katika shughuli zake na hatimaye kuondoa jamii kwenye umaskini unaotosababishwa na vitendo vya rushwa.

“Kazi zetu zinategemea taarifa na wananchi ndiyo wenye taarifa, hivyo tunafahamu umuhimu wa kuwaweka karibu na kuwapa elimu ili washiriki kikamilifu katika shughuli zetu,”anaeleza Kibwengo.

Kibwengo alidokeza kuwa ushiriki wao katika maonesho hayo ulilenga kutekeleza mkakati wa kitaifa,ambao unahimiza kushirikisha wadau wote wakiwemo wajasiriamali na wafanyabiashara ndogo, katika vita dhidi ya rushwa.

Naye Mkuu wa Dawati la Elimu la Takukuru mkoani hapa,Faustine Malecha, anafafanua zaidi kuhusu mkakati huo anasema unafahamika kama NACSAP III ambao utekelezaji wake ulianza Mwaka 2017 na unatarajiwa kukamilishwa Mwaka 2022.

Anasema lenga lake kuu ni kuwaondolea wananchi umaskini, kupiga vita vitendo vya rushwa na aliitaja kauli mbiu ya mkakati huo kuwa ni “Kata Mnyororo wa Rushwa Katika Ujasiriamali ili Kuboresha Mapato ya Wafanyabiashara,”

Kwa mujibu wa Machela,imebainika kuwa wananchi wengi hawafahamu vizuri majukumu ya taasisi hiyo,wengi wanadhani inakomea kuzuia na kupambana na rushwa tu.

Ingawa ni kweli kwamba majukumu yake ya msingi yapo manne na yamelenga zaidi kuzuia na kupambana na rushwa, Sheria Na. 11/2007 iliyoanzisha taasisi hiyo inaipa majukumu mengine ya kushughulikia jumla ya makosa mengine 24.

Anayataja majukumu manne hayo kuwa ni kuelimisha umma juu ya rushwa na athari zake, kuchunguza malalamiko ya rushwa, kukamata watuhumiwa wa rushwa na kuwafikisha mahakamani baada ya ushahidi kupatikana.

Majukumu mengineyo yaliyotajwa naye ni pamoja na kufanya utafiti kwenye idara za serikali na za binafsi,kufichua mbinu mpya zinazotumiwa kwenye vitendo vya rushwa kutokana na kwamba hubadilika, kulingana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Anasema sheria hiyo pia inaipa taasisi hiyo jukumu la kushughulikia makosa ya ubadhilifu wa mali za umma, matumizi mabaya ya ofisi (mamlaka/madaraka) pamoja na kuchambua miradi yote inayopelekwa kwenye halmashauri zote nchini.

Uchambuzi huo hulenga kuiwezesha kufahamu mambo yote yanayohusu miradi hiyo,ikiwa ni pamoja na kiasi cha fedha zilizopelekwa na kupokewa kwa ajili ya miradi husika.

“Tunatakiwa pia kufahamu nani amefadhili miradi, utekelezaji wake unatakiwa kukamilika ndani ya muda gani na hata wakati wa ukitekelezwaji wa mradi huwa tunanatakiwa kufatilia kwa karibu, ili kudhibiti matumizi ya fedha za umma,” anaeleza Machela.

KAULI ZA WAJASIRIMALI KUHUSU USHIRIKI WA TAKUKURU

Baadhi ya wajasiriamali waliozungumza na Majira kwenye maonesho hayo, walipongeza mpango huo wamba uliwarahisishia kuifikia na kunufaika na huduma zake.

Mjasiriamali kutoka Uyole -jijini Mbeya, Hoza Nkobokobo (63), anasema awali alidhani vitendo vya ngono kazini ni hufanyika kwa makubaliano kati ya wawili wanaohusika na hivyo haiwezekani kuwa moja ya aina mbalimbali za rushwa.

Lakini kupitia mafunzo aliyopata kutoka kwa wataalamu wa masuala ya rushwa wa TAKUKURU, akiwa mmoja wa wajasiriamali walioshiriki maonesho hayo, alielewa jinsi ambavyo mtu hususan mwenye mamlaka anavyoweza kutumia dhamana aliyopewa kutaka na kupata rushwa ya ngono kazini.

“Kumbe kazini kuna watu hasa wenye madaraka, wanaweza kutaka ngono na mtu hata kama hapendi, wakapata kwa sababu anayetakwa anaogopa kupoteza au kukosa maslahi yake,” anasema Nkobokobo.

Anasema alifanikiwa kuelimika hata bila kufika kwenye banda la maonesho la TAKUKURU,kwani maofisa wa taasisi hiyo walipokuwa wakipewa kipaza sauti walitoa elimu iliyomuwezesha kutoka hatua moja hadi nyingine kiuelewa.

Mjasiriamali mwingine kutoka Mwanza, Mussa Mchuma,alipongeza ubunifu wa taasisi hiyo wa kushiriki katika maonesho hayo kwani kwake ulimnufaisha kwa kuifikia kwa urahisi na kuhudumiwa.

Anasema isingekuwa rahisi kwake,kuacha maonesho yake ya bidhaa alizopeleka kwenda kutafuta ofisi zao zilipo ili kuomba ushauri aliokuwa akiuhitaji kwa muda mrefu.

Ingawa ufumbuzi wa tatizo alilokuwa nalo haukupatikana kwa asilimia 100, hatua zilizochukuliwa na maofisa waliokuwa wakiiwakilisha taasisi hiyo kwenye maonesho, zilimuondolea kabisa msongo wa mawazo aliokuwa nao.

Anaelezea kwa kifupi kuhusu tatizo lake kwamba anamiliki gari aina ya Coaster, ambayo aliikodisha kwa shule moja ya jijini Arusha lakini wateja wake hao hawakumpa malipo yake kwa muda mrefu, baadaye ikawa haionekani.

Anasema suala hilo alilifikisha mahakamani na kwamba yanayoendelea huko ndiyo yaliyokuwa yakimpa msongo wa mawazo, hali ambayo ilitoweka baada ya kushauriwa na maofisa wa TAKUKURU walikuwa kwenye maonesho hayo.

“Niliposikia matangazo yao, nikaona heri niende nikashauriwe kuhusu sarakasi nilizokutana nazo mahakama, nashukuru walinishauri na kuchukua maelezo yangu, wakanifungulia faili ambalo litapelekwa ofisini kwao Arusha…, nimefurahi sana,” anaeleza Mchuma.

Mchuma anasema awali hakufahamu kuwa TAKUKURU pamoja na kuzuia, kupambana na rushwa pia hufuatilia mienendo ya kiutendaji ya viongozi kwenye idara, taasisi na mamlaka mbalimbali serikalini na kwenye sekta binafsi.

Aliahidi kuwa balozi mzuri wa taasisi hiyo kwa wafanyabiashara wenzake, ambao anafahamu kuwa wanateseka kwa namna tofauti, wakikosa kimbilio kutokana na kutofahamu kwa undani majukumu ya Takukuru.

Aliomba jitihada zaidi zifanyike ili jamii ielimike na iweze kuitumia taasisi hiyo ipasavyo,kwani imejipambanua kuwa mtetezi wa wanyonge hasa katika kipindi hiki cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, ambayo inapinga unyanyasaji kwa watu wa kada la chini.