January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa:Tajirika na alizeti

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

JE, unataka kutajirika kupitia kilimo cha alizeti? Kama ndiyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ana ujumbe mahsusi kwako.

Anasema Waziri Mkuu Majaliwa: “Kama unataka utajiri wa haraka ndani ya miezi mitatu au minne, lima alizeti. Ukitaka fedha ya haraka, nzuri na ya uhakika na yenye faida kubwa lima alizeti. Kwa sababu kilimo chake si kigumu.”

Ujumbe huu wa Waziri Mkuu Majaliwa unatokana na umuhimu wa mafuta ya kula nchini na kwa ajili hiyo Serikali imeweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya mafuta yakiwemo chikichiki, alizeti, pamba, karanga na ufuta ili kujitosheleza na kuondokana na uagizaji mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi kwa mwaka hugharimu takribani sh. bilioni 474, fedha ambazo anasema zingeweza kuokolewa na zikapelekwa kwenye maeneo mengine yenye umuhimu mkubwa pia kama uboreshaji na utoaji wa huduma za afya, elimu na miundombinu.

Waziri Mkuu Majaliwa anasema mahitaji ya mafuta ya kula nchini yanakadiriwa kufikia tani 650,000 wakati uzalishaji wa ndani ni wastani wa tani 290,000 sawa na asilimia 45 ya mahitaji kwa mwaka. Nchi hulazimika kuagiza wastani wa tani 360,000 hadi tani 400,000 kwa mwaka kufidia upungufu huo.

Serikali imekuwa ikitoa kipaumbele katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo kuanzia ngazi ya uzalishaji, viwanda na masoko kutokana na ukweli kwamba takribani asilimia 70 ya Watanzania wanajishughulisha na kilimo. 

Juni 13, mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa ziarani mkoani Singida, alikutana na wadau wa zao la alizeti, lengo likiwa ni kuweka mikakati ya pamoja katika kuhakikisha nchi inaongeza uzalishaji na kuwa na kiasi toshelezi cha mafuta ya kula.

“Ni matarajio ya Serikali kuwa mikakati hiyo itawezesha kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa tani 649,437 hadi tani 1,500,000 za alizeti zitakazochangia upatikanaji wa mafuta kwa takribani tani 300,000 ifikapo 2025. Pia Serikali imeendelea kuwekeza katika taasisi zinazohusika na utafiti na uzalishaji wa mbegu ili kuongeza tija,” alisema Waziri Mkuu katika mkutano huo wa Singida.

Alisema baada ya Serikali kubaini kwamba inatumia fedha nyingi za kigeni katika kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi ilianza kutekeleza mikakati ya kuendeleza zao la michikichi kwa kuweka nguvu katika Mkoa wa Kigoma kwa kuanzisha kituo maalumu cha Utafiti wa Mchikichi cha Kihinga.

“Kupitia utafiti huo, tumeanza kuona matokeo makubwa ya uzalishaji wa miche bora yenye uwezo wa kuzalisha mafuta kiasi cha wastani wa tani 5 kwa hekta ikilinganishwa na aina ya michikichi ya zamani iliyopo sasa inayozalisha wastani wa mafuta ya mawese tani 1.6 kwa hekta,” alisema.

Na sasa alisema Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeamua kulipatia uzito unaostahili zao la alizeti kwa kuwaunganisha wadau na kuanzisha kampeni ya kilimo bora cha alizeti pamoja na kuhamasisha viwanda vya kukamua mafuta kwa kuboresha teknolojia kwa viwanda vilivyopo na kuanzisha viwanda vipya kulingana na mahitaji.

Katika kufanikisha mkakati huo, Mheshimiwa Majaliwa ameielekeza Wizara ya Kilimo iendelee kuwatambua wadau wanaowekeza kwenye zao la alizeti katika uzalishaji, viwanda na masoko na kuwaunganisha na wakulima na taasisi nyingine zikiwemo taasisi za fedha ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mitaji, masoko na malighafi kwa ajili ya viwanda vya mafuta.

Alisema Waziri Mkuu: “Wizara ya Kilimo, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa hakikisheni kuwa uzalishaji wa mazao ya mafuta hususan zao la alizeti unasimamiwa kikamilifu kwa kuweka mfumo thabiti wa usimamizi na ufuatiliaji katika ngazi zote.”

Mbali na agizo hilo pia Waziri Mkuu Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Kilimo na Maafisa Ushirika nchini washirikiane katika kusimamia kilimo cha zao la alizeti ili kuhakikisha malengo ya Serikali kuiwezesha nchi kuondokana na utegemezi wa kuagiza mafuta ya kula kutoka nje yanafikiwa.

Katika kuhakikisha lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao ya mafuta likiwemo zao la alizeti unafanikiwa nchini, Waziri Mkuu Majaliwa anasema kwa kuwa Maafisa Ugani na Maafisa Kilimo ndio hasa injini nyingine katika sekta ya kilimo yawapasa wawe na mashamba darasa.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada ya kubaini changamoto ya Maafisa Ugani wengi wasiokuwa na mashamba darasa, hivyo kushindwa kutoa mafunzo ya kilimo bora kwa wakulima.

Waziri Mkuu ameelekeza Wizara ya Kilimo na Ofisi ya Rais TAMISEMI ihakikishe maafisa hao wanasimamiwa kikamilifu ili watekeleze majukumu yao ipasavyo.

 “Maafisa Ugani lazima wawe na mashamba kwa ajili ya kufundishia wakulima na Afisa Ugani anayeshindwa kuonesha shamba huyo hafai kuwa Afisa Ugani,” anasema Waziri Mkuu.

Anaongeza: “Lengo la Serikali ni kuongeza uzalishaji na tija kwa kuimarisha utafiti, huduma za ugani, upatikanaji wa mbegu bora na viuatilifu, kuongeza matumizi ya zana bora za kilimo, kuwajengea uwezo wazalishaji kuhusu kanuni za kilimo bora, kuanzisha mfumo imara wa ugharamiaji wa mazao ya mafuta kwa kushirikisha taasisi za fedha.”

Waziri Mkuu anasema wananchi waliacha kulima alizeti kwa sababu elimu ilikuwa haiwafikii, hivyo amewaagiza Wakuu wa Wilaya katika maeneo yote yanayolima alizeti wasimamie uundwaji wa vikundi vya wakulima wa zao hilo.

“Vikundi ndiyo njia rahisi ya kuwafikia wakulima iwe kwa kuwapa elimu au mikopo. … Hakikisheni mnakuwa na kanzi data za wakulima katika maeneo yenu. Kanzi data hiyo itawawezesha kujua idadi ya wakulima, ukubwa wa mashamba yao pamoja na mahitaji yao. Jengeni pia utaratibu wa kuwatembelea wakulima ili kujua changamoto zinazowakabili na kushirikiana nao katika kuzitafutia ufumbuzi.”

Amewaagiza viongozi wa mikoa yote nchini waandae mpango mkakati wa kuendeleza mazao ya mafuta na kuuwasilisha Wizara ya Kilimo kwa ajili ya uratibu, usimamizi na ufuatiliaji ili “…kila kiongozi anapofanya ziara katika wilaya asomewe taarifa kuhusu hatua waliyofikia. Halmashauri za Wilaya zitenge maeneo ya kuzalisha mbegu bora na kuanzisha mashamba makubwa ya pamoja (block farms) ili kuongeza uzalishaji na kurahisisha utoaji wa huduma za ugani, mitaji na upatikanaji wa malighafi kwa viwanda vya mafuta ya kula.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amezielekeza taasisi za utafiti wa masuala ya kilimo ziendelee kufanya tafiti za udongo ili kubaini ni aina gani ya mbegu zinazofaa kupandwa kwenye eneo husika. Amesema tafiti zinawawezesha wakulima kupanda mbegu sahihi katika mashamba yao, hivyo kupata mavuno mengi na bora.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda anasema Serikali imeweka mkakati wa kuboresha huduma za ugani kwa kuongeza bajeti ili kuhakikisha wakulima wa zao la alizeti wanalima kilimo bora na kuongeza tija kwenye uzalishaji.

“Tumechagua Mikoa mitatu ya Dodoma, Singida na Simiyu kwa kuanzia kwa sababu ni Mikoa ambayo inalima mazao mbalimbali kwa ajili ya uzalishaji wa mafuta, ila kampeni hii ni ya nchi nzima na mikakati itakayowekwa ni kwa mikoa yote,” anasema Profesa Mkenda.

Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe anasema wizara imejipanga katika kuongeza uzalishaji wa mbegu bora kutoka tani 344 za sasa kufikia wastani wa tani 2,000 hadi 2,500 kwa mwaka, hivyo ndani ya miaka mitatu ijayo nchi itakuwa imejitosheleza kwa mahitaji ya mbegu za bora alizeti.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Binilith Mahenge aliiomba Serikali kuunda bodi itakayosimamia mazao ya mafuta ili kuboresha usimamizi wa mazao hayo.  Aliishauri pia Serikali kupitia taasisi zake kama Jeshi la Magereza zianzishe mashamba ya mbegu za alizeti ili kurahisisha upatikanaji wake.

Kwa upande wao wadau na wakulima wa zao la alizeti wakizungumza kwa nyakati tofauti katika kikao hicho waliiomba Serikali iwasaidie katika utoaji wa elimu kwa wakulima na elimu hiyo iambatane na kalenda itakayoonesha muda wa kuanzia kuandaa shamba hadi muda wa mavuno.

Waliomba pia Maafisa Kilimo washirikiane na wakulima katika kuwaelimisha namna bora ya kulima zao hilo ikiwemo matumizi ya mbegu bora pamoja na pembejeo ili waweze kuongeza tija na kuboresha maisha yao.