Na Mwandishi wetu,timesmajira,online
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuhakikisha inajenga uwiano mzuri wa kijinsia na wanawake katika uongozi na ngazi nyingine za maamuzi.
“Nitumie fursa hii pia kutambua mchango mkubwa wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kujenga uwiano wa kijinsia na wanawake katika uongozi”.
Amesema hayo leo (Jumatano, Novemba 10, 2021) alipomuwakilisha Rais Samia katika ufungaji wa Jukwaa la Uongozi wa Vijana kwa mwaka 2021 lilifanyika katika Chuo cha Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa (MS TCDC) jijini Arusha.
Amesema katika teuzi alizozifanya hivi karibuni, Mheshimiwa Rais Samia aliteua majaji wanawake 13 kati ya 28 wa Mahakama Kuu sawa na asilimia 43 na hivyo, kufanya idadi ya majaji wote nchini kufikia wanawake 40 kati ya majaji wote 86. “Ukiachilia mbali Katibu wa Bunge mwanamke, Mheshimiwa Rais pia aliteua Makatibu Tawala wa Mikoa wanawake 12 kati ya 26 sawa na asilimia 46”.
Mheshimiwa Majaliwa amesema Tanzania imeendelea kupiga hatua kubwa katika kuhakikisha inajenga uwiano mzuri wa kijinsia na wanawake katika uongozi na ngazi za maamuzi. “Kwa mfano katika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2015, tulikuwa na wabunge wanawake 127 ikilinganishwa na wabunge wanawake 143 mwaka 2020”
Waziri Mkuu amesema kuwa ili kukabiliana na changamoto ya ajira Tanzania iliamua kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kujenga uchumi wa kati wa viwanda na hivyo, kutengeneza ajira kwa kufungamanisha sekta hiyo na sekta nyingine za uchumi ikiwemo kilimo, madini, maliasili na utalii na sekta ya ujenzi.
Ameongeza kuwa juhudi hizo zimeonesha mafanikio baada ya Julai 2020 Tanzania kuingia kwenye kundi la nchi zenye uchumi wa kati wa chini. “Mafanikio hayo, yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na sera nzuri na fedha na uchumi jumla sambamba na matumizi sahihi ya rasilimali tulizo nazo na kuwa kwenye eneo la kimkakati kijiografia.”
Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa kwa wakuu wa nchi na Serikali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Umoja wa Afrika na sekta binafsi kuongeza juhudi katika kujenga usawa wa kijinsia na wanawake katika uongozi na ngazi nyingine za maamuzi.
Pia Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua mchango wa vijana katika kukuza uchumi hivyo ni muhimu vijana wakaendelea kujituma, kujitoa, na wawe waadilifu ili kujenga Taifa adilifu hasa wanaposhiriki katika matukio mbalimbali ya uzalishaji mali.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Peter Mathuki amesema atahakikisha anayafikisha mawazo yote yaliyotolewa na vijana hao kwa watunga sera katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ili yaweze kufanyiwa kazi kwa maendeleo ya vijana na jumuiya kwa ujumla.
Kadhalika, kiongozi huyo amewaomba viongozi mbalimbali waendelee kuwafundisha na kushirikiana na vijana hao ili waweze kujifunza zaidi na kuwa viongozi bora hapo baadaye.
More Stories
Wenje:Tuwanadi wagombea bila kuchafuana
Mtoto darasa la tatu adaiwa kujinyonga kwa kukosa nguo ya sikukuu
Jeshi la Polisi Katavi laanika mafanikio 2024