Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa,amesisitiza na kuelekeza,mambo saba yatakayochangia kuboresha hali ya lishe nchini na kuondoa changamoto,zinazoikabili sekta hiyo.
Kwani lishe ni moja ya vipaumbele muhimu kwa Serikali, kuwezesha kutekeleza mipango ya kuwaletea wananchi maendeleo na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii,ikiwemo kilimo, uvuvi, ufugaji na biashara.
Majaliwa amesisitiza mambo hayo, Oktoba 3,2024,wakati akifunga mkutano wa 10,wa wadau wa lishe nchini,uliofanyika kwa siku mbili wilayani Ilemela mkoani Mwanza.Wenye kauli mbiu”Kuchangiza mchango wa wadau wa kisekta,ili kudumisha matokeo bora ya hali ya lishe nchini Tanzania”.
Ambapo moja ya jambo alilosisitiza ni pamoja na wadau wote wa lishe,wahikishe wanatumia vizuri ,matokeo ya ripoti ya muda wa kati, ili kujitathmini na kuchukua hatua stahiki za kuboresha utekelezaji wa afua za lishe,kwa kipindi kilichobaki cha mpango wa taifa wa lishe.
Huku jambo jingine alilosisitiza ni wadau wote watekeleze kikamilifu maazimio ya mkutano huo wa kumi wa wadau wa lishe, ili kuimarisha utekelezaji wa mpango jumuishi wa taifa wa lishe.
Pia,amezitaka Wizara,wakala,taasisi na mashirika ya umma,watumie kikamilifu mwongozo wa mpango jumuishi wa taifa wa lishe na bajeti, kuhakikisha masuala ya lishe yanajumuishwa katika mipango na kutengewa fedha ili yatekelezwe kikamilifu kila mwaka.
Huku Mikoa na Halmashauri,watumie vizuri mwongozo wa kitaifa wa utoaji wa huduma ya chakula na lishe kwa wanafunzi wa elimu ya msingi, na kuhakikisha matumizi ya vyakula vilivyorutubishwa yanajumuishwa na kutengewa fedha katika mipango na bajeti za kila mwaka.
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu,(Sera,Bunge na Uratibu),William Lukuvi,amesema,utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (2022),zinaonesha viwango vya udumavu na uzito mdogo (underweight) kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano, vimekuwa vikipungua.
Ambapo katika kipindi cha mwaka 2018 na 2022,udumavu ulipungua kutoka asilimia 32 iliyokuwa mwaka 2018 hadi asilimia 30 kwa mwaka 2022.Huku uzito mdogo ulipungua kutoka asilimia 16 hadi asilimia 12 katika kipindi hicho.
Kwa upande wake Katibu Mkuu,Ofisi ya Waziri Mkuu(Sera,Bunge na Uratibu),Dkt.Jim Yonazi,amesema mkutano wa wadau na wataalamu wa lishe uliofanyika Oktoba 2,2024, kupitia majadiliano yalipatikana maazimio matano, ikiwemo masuala ya huduma za lishe yajumuishwe katika dira ya taifa ya mwaka 2050.
Naye Meneja Mradi wa Afya na Lishe kwa kuzingatia usawa wa kijinsia,wa shirika la Word Vision Tanzania, Shukrani Dickson, amesema katika suala la lishe ,Tanzania bado ipo chini hasa katika udumavu na utapiamlo kwa watoto.
“Tunawafundisha wakina mama, namna ya kuandaa mlo kwa ajili ya watoto,tunahakikisha kila mwaka,watoto wanapata chanjo ya vitamin ‘A’.Na kuwawezesha wahudumu wa afya kutembelea kaya kwa kaya,ili kuwafundisha wakina mama jinsi ya kuwatunza watoto,kuhudhuria kliniki na kuwapima,”ameeleza Shukrani na kuongeza:
“Word Vision Tanzania,tunao mpango wa kuhamasisha watu kulima viazi lishe na maharage lishe, ambavyo vinaongeza sana virutubisho kwa watoto,kwa kuwapatia mbegu,elimu na utaalamu mbalimbali,ili kukabiliana na changamoto ya lishe duni,”.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best